Na Edina Malekela na Boniphace Jilili,Singida.
MWENYEKITI wa Kamati ya usalama barabarani Mkoa wa Singida Elias Seng'ongo amewaomba watumiaji wote wa barabara kushirikiana na jeshi la Polisi katika kuondoa ajali zinazoendelea kujitokeza maeneo mbalimbali hapa nchini. Seng'ongo alitoa rai hiyo leo wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani,shughuli iliyokwenda sambamba na ukaguzi wa mabasi ambapo ilifanyika kituo kikuu cha mabasi cha Misuna mjini Singida.
Alisema kila mmoja akichukua hatua ya kuchukua tahadhari kuanzia madereva na watumiaji wengine wa barabara pamoja na wasimamizi wa Sheria (askari) ajali zitaepukika hivyo wachukue hatua hizo hasa ikizingatiwa ni mwisho wa mwaka kwani ajali nyingi hutokea.
Awali mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Singida SSP Nestory Didi alisema wiki ya nenda kwa usalama barabarani haishughuliki tu na watumiaji wa barabara bali pia inashughulika na wasimamizi wa sheria ambao ni askari,hivyo Jeshi la Polisi linahakikisha linawapiga msasa maaskari wake katika usimamizi wa sheriaili uwe wa haki.
"Katika wiki hii tutahakikisha tunawapiga msasa askari wetu ili kuondoa malalamiko yanayojitokeza ili kuleta tija na ufanisi katika utendaji wao wa kazi." alisema Didi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha madereva na wamiliki wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu nchini (CHAMWAPITA) Michael Haule alishauri wiki ya nenda kwa usalama barabarani iwe inafanyika mara mbili kwa mwaka kutokana na changamoto za ajali zinazoendelea kujitokeza ili watumiaji wa barabara wapate elimu.
Aidha alisema ukaguzi wa magari unaofanyika kwenye wiki ya nenda kwa usalama barabarani uwe endelevu badala ya wiki husika pekee jambo litakalosaidia kuondoa ajali kutokana na watumiaji kukumbushwa mara kwa mara,hivyo hawatasahau.
Ametaka madereva wanaovunja sheria kuchukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kunyang'nywa leseni ili iwe fundisho kwa wengine na itasaidia kuondoa ajali ambazo sio za lazima zile za kujitakia.
Ukaguzi wa mabasi wa mabasi ukiendelea.
Mkaguzi wa magari na mtahini wa Madereva kutoka ofisi ya RTO Inspector Stephen Nyandongo akielezea namna kikosi cha usalama barabarani kinavyofanya kazi zake kwa weledi.
Mkuu wa Polisi kikosi cha usalama Barabarani Mkoa wa Singida katikati SSP Nestory Didi akiwa kwenye banda la maonyesho kwenye siku ya usalama barabarani iliyofanyika katika stendi kuu ya mabasi Misuna mkoani Singida.
Mwenyekiti wa kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Singida Elias Seng'ongo akihutubia hadhara.
Social Plugin