WABUNGE WATEMBELEA BANDA LA HAKIRASILIMALI..CHAGONJA AELEZEA UTAJIRI WA TANZANIA


Mkurugenzi wa HakiRasilimali Racheal Chagonja akiwaelezea baadhi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, namna wanavyofanya kazi zao katika Sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi, walipofika kwenye Banda hilo katika maonesho ya wiki ya Azaki Jijini Dodoma.


Na Marco Maduhu, DODOMA

ASASI ya HakiRasilimali ambayo inajihusha na Sekta ya uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi, imeendelea kuonyesha kazi zao kwenye wiki ya Asasi za kiraia (AZAKI) Jijini Dodoma, ambapo watu mbalimbali wakiwemo viongozi na wabunge wametembelea banda la asasi hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Kwela Sumbawanga mkoani Rukwa Mhe. Deus Sangu, pamoja na Mbunge Jimbo la Busanda mkoani Geita Mhe, Tumaini Magessa, wameizungumzia Sekta ya uziduaji namna inavyoweza kuleta utajiri kwa Watanzania na kukuza pato la Taifa.

Mbunge wa Jimbo la Kwela Mhe Sangu,akiwa  kwenye banda la HakiRasilimali, amesema Gesi ya Helium inayotarajiwa kuzalishwa katika bonde la Ziwa Rukwa mkoani Rukwa, ina uwezo wa kuuzwa kwenye Soko la dunia kwa miaka 20 ijayo.

Amesema Mkoa wa Rukwa una utajiri mkubwa wa Gesi ya Helium, na kwamba mara baada ya mradi kukamilika gesi hiyo, utaliingizia kipato kikubwa Taifa kutokana na uuzaji katika soko la dunia.

Ameongeza kuwa kwa sasa Marekani ndiyo inayoongoza katika uuzaji wa Gesi ya Helium, na kwamba mara baada ya kukamilika kwa mradi huo wa Bonde la Rukwa, Tanzania itaingia katika soko la dunia kuuza Rasilimali hiyo.

Aidha Mhe. Sangu, ameiomba Wizara ya Nishati kufanya ziara za mara kwa mara mkoani Rukwa, ili kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha ili watambue umuhimu wa gesi hiyo na faida yake kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja kuwainua kiuchumi na Taifa kwa ujumla.

Katika hatua nyingine Mhe. Sangu amebainisha changamoto zilizopo kwa sasa katika mradi huo, kuwa ni pamoja na ubovu wa barabara, ushirikishwa wa wananchi, pamoja na wazawa kukosa ajira ndogo ndogo ambazo zinatolewa kwa watu kutoka nje ya maeneo ya mradi.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Busanda mkoani Geita Mhe Magessa, naye akizungumza kwenye banda hilo la HakiRasilimali, amesema, kuna haja ya kuwa na kampeni ya nchi nzima kuhamasisha ufungamanishaji wa Sekta ya madini na Sekta nyingine hususani kilimo ili kuwa na uchumi endelevu.

"Katika maeneo ninayotoka shughuli za uchimbaji wa Madini ya dhahabu zimekuza Miji na kuimarisha Biashara,” amesema Magessa na kuongeza kuwa,

"Katika maeneo ya uchimbaji madini, kilimo bado hakijapewa kipaumbele sana yani bado haki ridhishi ambapo kuna haja ya kufanyiwa kampeni ili kufungamanisha Sekta hizi mbili madini na kilimo na kuinua uchumi wa Watanzania sababu kilimo ndiyo nguzo kuu ya uchumi.”

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa HakiRasilimali Racheal Chagonja, amesema nchi ya Tanzania ina utajiri mkubwa, na kubainisha kuwa Rasilimali za nchi ni vyema zikawanufaisha wananchi wenyewe, na kwamba Elimu itolewe kwa wananchi ili kila mmoja afahamu utajiri wa Rasilimali katika eneo analoishi.

Mradi wa Gesi wa Helium katika Bonde la Ziwa Rukwa umeanza mwaka 2016 una mita za ujazo zipatazo Bilioni 98 ambao kwa sasa upo katika hatua za awali za ujenzi.


Mbunge wa Jimbo la Kwela Sumbawanga mkoani Rukwa Mhe. Deus Sangu,akizungumzia Sekta ya Uziduaji kwenye Banda la HakiRasilimali katika wiki ya Azaki Jijini Dodoma.

Mbunge wa Jimbo la Busanda mkoani Geita Mhe Magessa, akizungumzia Sekta ya Uziduaji kufangamanishwa na Kilimo kwenye Banda la HakiRasilimali katika wiki ya Azaki Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa HakiRasilimali Racheal Chagonja akiwaelezea baadhi ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania namna wanavyofanya kazi zao za Sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi, wakati walipofika kwenye Banda hilo katika maonesho ya wiki ya Azaki Jijini Dodoma.

Wabunge wakiendelea kumsikiliza Mkurugenzi wa HakiRasilimali Racheal Chagonja.

Baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwa kwenye Banda la HakiRasilimali, wakimsikiliza Mkurugenzi Asasi ya HakiRasilimali Racheal Chagonja, akielezea Sekta ya Uziduaji kwenye Madini, Mafuta na Gesi.

Awali Mkurugenzi wa HakiRasilimali Racheal Chagonja, (kushoto) akiwakaribisha baadhi ya wabunge kwenye Banda la HakiRasilimali walipotembelea banda hilo katika kuadhimisha wiki ya Asasi za kiraia.

Wabunge wakimsikiliza Katibu wa Chama cha wachimbaji wa madini wanawake Tanzania (TAWOMA), Salima Ernest akielezea namna wanavyoongeza Thamani ya madini kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa kutumia madini.

Baadhi ya wafanyakazi wa HakiRasilimali wakiendelea kueleza wananchi mbalimbali ambao wamefika kwenye banda hilo namna wanavyofanya shughuli zao katika Sekta ya Uziduaji.

Na Marco Maduhu, DODOMA.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post