Na Dinna Maningo, TARIME.
MABADILIKO ya hali ya hewa yamesababisha athari za Kiuchumi na Kijamii huku Serikali ya Nchi ya Tanzania ikitumia fedha nyingi kugharamia majanga vikiwemo vifo,upotevu wa mali,uharibifu wa mazao,mifigo miundombinu ya barabara,maji na umeme.
Sekta zote za kiuchumi na kijamii zimeendelea kuathirika na zitaendelea kuathirika kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa,sekta ambazo zimeathirika zaidi ni pamoja na Kilimo,Maji,Mifugo,Nishati,Uvuvi,Usafirishaji na Afya.
Hayo yameelezwa katika kijarida Sera cha kusambaza matokeo ya utafiti kilichoandaliwa na watafiti kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwakushirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Kwa mujibu wa utafiti Kitengo cha Maafa (Disaster Management) zinaonyesha kuwa katika miaka 20 iliyopita kuanzia 2000 hadi 2019,Serikali imetumia kiasi cha Dolla za Kimarekani Milioni 20.5 kugharamia majanga mbalimbali yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa.
Takwimu za utafiti zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2000 hadi 2019 takribani nyumba 35,730 ziliharibiwa na Kaya 25,640 ziliathirika na kusababisha vifo 450 na watu 240 waliumizwa.
Mfano dhahili wa madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa ni mafuriko yaliyotokea mkoa wa Dar es salaam mwaka 2011/2012 ambayo yalisababisha vifo vya watu 43 na uharibifu wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya maji,barabara na umeme.
Gharama za uharibifu huo zinakisiwa kufikia shilingi milioni 7.5 huku serikali ikitumia kiasi cha shilingi Bilioni 1.8 kuwaokoa watu na kuwahamisha kutoka maeneo ya mabondeni na kuwapeleka maeneo ya Mabwepande.
Thathimini ya kisayansi zinaonyesha kuwa matokeo ya vipindi vya hali mbaya ya hewa yakiwemo matukio ya ukame,mafuriko,na vipindi vifupi vya mvua kubwa na upepo mkali vimeendelea kuongezeka nakusababisha athari za kiuchumi na kijamii.
Athari zingine zinazoendelea kujitokeza ni pamoja kuongezeka kwa kina cha maji ya baharini kwenye ukanda wa pwani kwa wastani wa milimita 3.24 kwa mwaka,kuongezeka kwa magonjwa ya mazao ya kilimo na mifugo.
Tafiti zinaeleza kuwa joto linatarajiwa kuongezeka kwa nyuzi joto 2°C mpaka 4°C katika maeneo mbalimbali nchini,matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa,mafuriko,upepo mkali na ukame yanatarajiwa kuongezeka katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Imebainika kuwa joto la mchana linatarajiwa kuendelea kuongezeka katika mikoa yote ya Tanzania,joto la usiku linatarajia kuongezeka katika mikoa yote ya Tanzania,kasi ya ongezeko lake linatarajiwa kuwa kubwa zaidi kuliko joto la mchana,maeneo ya magharibi mwa nchi,nyanda za kusini magharibi na upande wa Mashariki mwa Ziwa Nyasa yanatarajiwa kuwa na ongezeko la joto la juu kiasi cha nyuzi 3.5°C.
Tafiti zinaonyesha kuwa maeneo ya Ziwa Victoria,na baadhi ya sehemu ya nyanda za juu kaskazini mashariki yanatarajiwa kuongezeka kwa joto la chini kwa kiasi cha nyuzi joto 4.5°C mpaka 4.8°C,hivyo msimu wa baridi inayoanzia mwezi Julai mpaka Septemba inatarajiwa kuwa na joto la juu kuliko ilivyozoeleka huko nyuma (baridi kidogo).
Upande wa maeneo ya kusini,nyanda za juu kusini na maeneo ya magharibi mwa nchi mvua zinatarajiwa kupungua. Hata hivyo ongezeko la mvua linatarajiwa kuchangiwa zaidi na matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa na sio kwa mtawanyiko mzuri wa mvua.
Kwa mujibu wa watafiti wanasema kuwa kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa duniani kote inaendelea kuongezeka kila mwaka na athari zake katika sekta zote za kiuchumi na kijamii zinaendelea kuwa kubwa hususani kwa nchi zinazoendelea ambazo uwezo wake wa kuhimili na kukabiliana na athari hizo ni ndogo.
Tafiti zinaonyesha kuwa kwa mujibu wa ripoti iliyofanywa na jopo la kiserikali lenye dhamana ya kutoa tathimini ya kisayansi ya mwelekeo wa mabadiliko ya hali ya hewa inaonesha kuwa wastani wa ongezeko la joto duniani unatarajiwa kufikia nyuzi joto 1.5 kati ya mwaka 2030 na 2052,endapo kasi ya mabadiliko itaendelea kwa viwango vya sasa.
Tafiti zinaeleza kuwa kutokana na ongezeko la madhara yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa,serikali kupitia ofisi ya makamu wa Rais kitengo cha Mazingira iliandaa mpango mkakati kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa mwaka 2012.
Mkakati wa mpango huo unaelezwa kuwa umesaidia kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa kuijengea jamii uelewa na kutekeleza baadhi ya miradi ya kupunguza athari ikiwemo ujenzi wa uzio ufukweni mwa bahari ya Hindi,mradi wa mabasi ya mwendokasi,mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme (Julius Nyerere Hydropower Dam) unaotarajiwa kukamilika 2022, ukikamilika utazalisha umeme wa MW 2115.
Imeelezwa kuwa Serikali imeendelea kuimarisha uangalizi wa hali ya hewa kwa kununua na kusimika rada za hali ya hewa ambazo zimesaidia kuongeza ufanisi wa ufuatiliaji wa vimbunga.
Ili kuongeza uwezo wa Taifa na Jamii yote ya Watanzania wa kuhimili na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa watafiti wamependekeza elimu itolewe kwa jamii kuhusiana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa,kuimarisha mifumo ya uangalizi wa matukio hayo kabla hayajatokea.
Imeelezwa kuwa jitihada ziendelee kufanyika ili kuimarisha usambazaji wa taarifa za hali ya hewa ili ziwafikie walengwa,kuimarisha utafiti wa mifumo ya hali ya hewa na mabadiliko yake,kuwepo wa Sera ya hali ya hewa utaongeza tija na ufanisi katika matumizi ya taarifa na kujenga uelewa na utekelezaji wa sheria ya hali ya hewa Namba 2 ya mwaka 2019.
Watafiti wanapendekeza na kuhitimisha kuwa,kuwepo kwa mkakati wa kitaifa wa kuimarisha kilimo na maendeleo ya viwanda vya ndani,upatikanaji wa mbegu bora zinazostahimili ukame, dawa, pembejeo.
Kuwepo kwa ushirikiano baina ya Taasisi ya Kilimo ( TARI),Taasisi ya Mifugo (TALIRI) Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),Tume ya Tarifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH)na Taasisi zingine za utafiti na kuboresha namna ya kusambaza Teknolojia ma matokeo ya tafiti zinazotoa majibu ya changamoto za wakulima,wavuvi na wafugaji nchini.
Social Plugin