MAPENZI ni upofu na Waswahili wanasema kipenda roho hula njama mbichi! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia tukio lililogusa mioyo ya wengi, ambapo mwanadada Deborah Muteteri au maarufu kwa jina la Borah, amekubali kuendelea kuishi na mumewe, Ndayisenga Jean baada ya kugundua kwamba mwanaume huyo hakuwa na miguu, jambo ambalo alimficha.
Debora aligundua kwamba mumewe hana miguu, usiku wa siku yao ya harusi baada ya mwanaume huyo kuamua kumfichulia siri ambayo alikuwa akiificha kwa kipindi chote tangu walipokutana na kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Wakizungumza na Kituo cha Runinga ya Mtandaoni cha Afrimax, wawili hao wameeleza jinsi walivyokutana mpaka siku yao ya harusi, na kilichoendelea baada ya mwanamke huyo kugundua kwamba mumewe alikuwa amemficha jambo kubwa kiasi hicho.
Akielezea historia yake, Ndayisenga anasema alizaliwa akiwa mzima lakini alipofikisha umri wa miaka saba, familia yao ilikimbilia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, baada ya vita kuzuka nchini humo.
Familia hiyo iliendelea kuishi uhamishoni na baada ya hali ya kiusalama kutulia, iliamua kurudi nchini Rwanda lakini kwa bahati mbaya, Ndayisenga, wazazi wake na ndugu zake wengine wakiwa njiani, bomu lililipuka na kumsababishia ulemavu wa kudumu.
Anaeleza kwamba katika tukio hilo, kitu anachokumbuka ni kwamba walikuwa ndani ya gari, bomu likalipuka na kusababisha kishindo kikubwa lakini baada ya hapo, hakuelewa tena kilichoendelea, mpaka alipokuja kuzinduka na kujikuta akiwa hospitalini.
Anaeleza kuwa madaktari walimueleza kwamba alikuwa kwenye usingizi wa kifo, Coma kwa kipindi cha miezi miwili, jambo ambalo lilimshangaza mno.
Anazidi kueleza kuwa mshtuko wake ulizidi baada ya kugundua kwamba mguu wake mmoja ulikuwa umekatwa, ambapo madaktari walimueleza kuwa waliukata mguu huo kutokana na kuharibika vibaya kufuatia kulipukiwa na bomu, hilo likawa pigo la kwanza katika maisha yake.
Wiki chache baadaye, madaktari walimueleza tena Ndayisenga kwamba mguu wake mmoja uliosalia, nao unatakiwa kukatwa kwani ulishaanza kuonesha dalili za kansa, hatimaye mguu huo nao ukakatwa na kumuacha akiwa na ulemavu wa kudumu.
Anaeleza kwamba maisha yake yalipoteza kabisa mwelekeo kwani bado alikuwa mdogo, akiwa na umri wa miaka saba tu, lakini mama yake akawa mfariji mkubwa katika maisha yake.
Maisha yaliendelea lakini kama Waswahili wanavyosema, mbuzi wa maskini hazai! Mama yake ambaye ndiye aliyekuwa tegemeo lake, alipata ujauzito na kwa bahati mbaya mtoto akafia tumboni, jambo lililomfanya augue sana na baadaye, naye akapoteza maisha.
Mtu pekee ambaye sasa alibaki kuwa tegemeo kwenye maisha ya Ndayisenga, alikuwa ni baba yake ambaye naye, alianza kuumwa na hatimaye akafariki dunia, na kumuacha Ndayisenga akiwa na mdogo wake wa kike ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka mitatu tu.
Anazidi kueleza kwamba maisha yalikuwa magumu sana kwake na kwa mdogo wake, mitaani nako watu wakawa wanamnyanyapaa kwa sababu ya ulemavu wake na anaeleza kwamba kuna kipindi kilifika akatamani kuyakatisha maisha yake.
Kwa bahati nzuri, alikutana na watawa wa kanisa moja nchini humo ambao waliamua kumsaidia, wakampeleka hospitali na baada ya vipimo, madaktari wakashauri kwamba awekewe miguu ya bandia, hilo likafanyika kwa gharama za watawa hao.
Miguu hiyo ya bandia ilimpa kijana huyo nguvu mpya ya kusimama na kuanza kuzifukuzia ndoto zake, akaendelea na masomo yake. Miaka kadhaa baadaye, aligundua kwamba alikuwa na kipaji cha kuimba na safari yake hiyo mpya ya usanii, ndiyo iliyokuja kumkutanisha na mwanamke wa maisha yake, Debora.
Ndayisenga anaeleza kwamba anakumbuka kulitokea mashindano ya kuimba, kwa kuwa alikuwa na kipaji na yeye akaenda kushiriki.
Zamu yake ilipofika alionesha kipaji chake na wengi walionesha kuvutiwa na uwezo mkubwa aliokuwa nao. Debora alikuwa miongoni mwa watu waliofurahishwa na kipaji chake, ni hapo ndipo walipokutana kwa mara ya kwanza baada ya Ndayisenga kushuka jukwaani, wakabadilishana namba za simu na mawasiliano yakaanzia hapo.
Baada ya mawasiliano kuzidi kushika kasi, miezi mitano baadaye, waliingia rasmi katika uhusiano wa kimapenzi na makubaliano yao yalikuwa ni kwamba hawatakiwi kufanya chochote mpaka watakapofunga ndoa.
Baada ya kusomana vya kutosha, hatimaye wawili hao walitangaza ndoa, maandalizi yakafanyika na hatimaye wakafunga ndoa na kuwa mume na mke halali! Usiku wa siku ya harusi yao, ndipo Ndayisenga alimpomueleza ukweli mwanamke huyo, ikiwa ni pamoja na kuvua miguu ya bandia aliyokuwa akiitumia siku zote, ikawa ni sapraiz kubwa kwa bibi harusi.
Alimueleza kwamba aliamua kuificha siri hiyo kwa sababu aliogopa kwamba huenda mwanamke huyo anaweza kumkataa kwa sababu ya ulemavu wake, na kumrudisha kwenye maisha ya upweke ambayo yalishauchosha moyo wake.
Akizungumzia jinsi alivyopokea taarifa hizo, Deborah anasema kwanza alishtuka kwa sababu ni jambo ambalo hakulitegemea, lakini baada ya kuujua ukweli, alijiona kwamba ana jukumu kubwa la kumuonesha upendo zaidi Ndayisenga kuliko hata ilivyokuwa mwanzo, ili amsahaulishe mambo yote mabaya aliyowahi kuyapitia.
Mwanadada huyo ananukuliwa akisema, baada ya kunionesha jinsi miguu yake ilivyokuwa, nilipata sababu milioni moja za kuzidi kumpenda zaidi. Kitendo hicho kilinipa nguvu za ajabu. Nikagundua kwamba natakiwa kufanya zaidi kwa ajili yake ili awe na furaha na asahau yote aliyopitia.
Anazidi kueleza kuwa, watu wengi walimshangaa kutokana na uamuzi wake wa kuendelea kuishi na mwanaume huyo hata baada ya kuujua ukweli, wengi wakimshauri aachane naye kwa kuwa ni mlemavu na atafute mwanaume mwingine mwenye fedha, majumba na magari lakini kamwe hakutaka kumsikiliza yeyote!
Basi ukisikia mapenzi yana nguvu, ndiyo kama hivyo ulivyosikia! Ni miezi takribani nane sasa tangu wawili hao walipofunga ndoa na wanaendelea na maisha yao, huku wakioneshana mapenzi motomoto!
Social Plugin