BILIONI 18.8 KUTUMIKA KUJENGA OFISI YA MAKAMU WA RAIS JIJINI DODOMA
Wednesday, October 13, 2021
Ofisi ya Makamu wa Rais imesaini Mkataba wa Shilingi Bilioni 18.8 na Kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT wa kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Hafla ya kusaini Mkataba wa ujenzi huo imefanyika katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mtumba jijini Dodoma Oktoba 13, 2021 na kukabidhi rasmi eneo la ujenzi kwa Mkandarasi baada ya kushinda zabuni, na kushuhudiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambaye ndio Msimamizi Elekezi wa ujenzi wa jengo hilo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga ameipongeza SUMA JKT kwa kushinda kandarasi hiyo na kutaka ujenzi uwe wa haraka kwa kuzingatia ubora, viwango na kasi.
“Ninaamini kuwa SUMA JKT mna uzoefu mkubwa, na ujenzi huu utaenda kwa kasi, na kuzingatia viwango vya ubora wa hali ya juu, na ikiwezekana mkamilishe kazi hii kabla ya muda uliopangwa,” amesema Bi. Mary Maganga.
Aidha, Katibu Mkuu alisema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kwa kuwa Serikali ilipohamia Dodoma jengo lililojengwa katika eneo la Mtumba halitoshelezi mahitaji ya watumishi wote hivyo kulazimika kutumia jengo lingine mjini kwa ajili ya watumishi wa idara zingine.
“Wenzetu wa Idara ya Mazingira wapo wengi na wana majukumu mengi kila tunapowahitaji kuja kwa ajili vikao inabidi waje huku Mtumba kwa hiyo jengo hili likikamilika ndani ya muda tuna imani ufanisi utaongezeka na tunaweza kufanya kazi kwa pamoja na muda tunaotumia barabarani utapungua au kuondoka kabisa,” alisema.
Aidha, Bi. Mary Maganga amesema, msimamizi wa ujenzi huo Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) atafanya kazi kwa karibu na Kamati ya Ujenzi ya Ofisi ya Makamu wa Rais inayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Bw. Mohammed Khamis Abdullah na kusisitiza kutenga Ofisi kwa ajili ya Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
“Ofisi ya Makamu wa Rais ndio wasimamizi wa Masuala ya Muungano na Mazingira hapa nchini, hivyo tutatoa nafasi katika jengo hili jipya kwa ajijli ya wenzetu wa Ofisi ya Uratibu wa Shughuli za Serikali kwa upande wa Zanzibar kupata nafasi ili kurahisisha masuala ya uratibu wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa pande zote mbili za Muungano.” ameongeza Bi. Mary Maganga.
Naye, Mhandisi Morgan Nyonyi kutoka SUMA JKT amemthibitishia Bi. Mary Maganga kuwa, SUMA JKT watatekeleza mradi huo kwa ustadi mkubwa kwa kuhakikisha wanakailisha mradi huo wa ujenzi kwa wakati na ikiwezekana kabla ya miezi 24 iliyopo ndani ya Mkataba.
“Tutajitahidi kwenda na wakati na kuzingatia viwango vya ubora, rasilimali fedha na rasilimali watu tunao wa kutosha. Naishukuru Serikali kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha zitakazowezesha kutekelezwa kwa mradi huu na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutuamini SUMA JKT” Alisisitiza Mhandisi Nyonyi.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za Kihandisi wa NHC, Mhandisi Manning Mwalaka, amesema Shirika litahakikisha Mkandarasi anafuata taratibu zote za ujenzi kwa mujibu wa mkataba katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.
“Sisi na NHC tumepewa dhamana ya kuwa wasimamizi katika mradi huu, tutashirikiana kwa pamoja, na kuhakikisha kwamba hili jengo linajengwa kwa viwango vilivyokusudiwa,” ameeleza Mhandisi Mwalaka.
Kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo, kutapelekea Idara na Vitengo vyote vya Ofisi ya Makamu wa Rais kuhamia katika jengo hilo.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin