Na Mwandishi Wetu
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa muda wa siku nne kuanzia Oktoba 4-7, mwaka huu kwa wanafunzi 2,982 walioomba mikopo kwa mwaka 2021/2022 kufanya marekebisho ili kukamilisha taratibu za maombi yao.
Ili kupata taarifa za kina kuhusu marekebisho hayo, waombaji husika wameshauriwa kutembelea akaunti zao walizotumia kuomba mkopo kwa njia ya mtandao maarufu kama SIPA-Student’s Individual Permanent Account (SIPA).
Soma Pia: Majina ya waliokosea fomu za bodi ya mikopo 2021/2022
Akizungumza katika mahojiano maalum na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo HESLB, Dkt. Veronica Nyahende alisema mara baada ya kukamilika kwa hatua hiyo ya marekebisho, HESLB itaanza kuwapangia mikopo wanafunzi wahitaji.
“Katika uhakiki wa maombi tumebaini waombaji 2,982 fomu zao zina kasoro. Tumetoa muda wa siku nne, na baada ya hatua hiyo kukamilika tutaanza mchakato wa kupanga mikopo kwa wanafunzi wenye sifa na uhitaji”, alisema Dkt. Nyahende.
Soma Pia: How to Correct HESLB loan Application forms 2021/2022
Kwa mujibu wa Dkt. Nyahende waombaji pia watapaswa kutembelea akaunti za SIPA ili kupata taarifa za mikopo watakayopangiwa na HESLB baadaye mwezi huu.
Hadi kufikia Septemba 30, mwaka huu, HESLB ilikuwa imepokea maombi 88,688 na kati ya maombi hayo; 85,706 yalikuwa kamilifu na 2,982 yalitakiwa kufanyiwa marekebisho.
Dkt. Nyahende aliongeza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha fedha za mikopo ya wanafunzi zinalipwa kabla ya vyuo vya elimu ya juu kuanza kufunguliwa kuanzia Oktoba 25 mwaka huu.
Soma Pia: HESLB Appeal Guidelines 2021/2022
Katika mwaka wa masomo 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha TZS 570 Bilioni kwa ajili ya bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu 162,000 wakiwemo wanafunzi 62,000 wa mwaka wa kwanza na 98,000 wanaoendelea na masomo.
Social Plugin