Katibu wa CCM
Kata ya Mandewa Yusuph Kijanga (kushoto)
akifurahia jambo wakati alipo wasili kwenye ofisi za Shule ya Msingi Mwaja kwa ziara ya kichama.
Kulia aliyemshika mkono ni Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Shorisael Mosses.
Mwonekano wa darasa jipya
la Shule ya Utayari Kitope linalojengwa kwa nguvu ya wananchi ambapo maombi maalumu yamewasilishwa kwa Kamati ya Siasaya
Kata
ya Mandewa kuomba baada ya kukamilika kwake shule hiyo itambuliwe rasmi kuwa Shule Shikizi ya Shule ya Msingi Mwaja iliyopo ndani ya
kata hiyo.
Mwonekano wa miradi ya miundombinu mipya inayoendelea ya madarasa kwenye baadhi ya madarasa ndani ya
kata hiyo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mandewa Georgia Maghiya akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Mandewa mwonekano wa ujenzi wa bweni jipya la wasichana unaoendelea. Shule hiyo ya sekondari pekee ndani ya kata hiyo mwakani inatarajia kuanza kutoa masomo ya Kidato cha Tano na Sita (A Level Studies)
Na Godwin Myovela, Singida
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Mandewa mkoani hapa imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maboresho ya miundombinu ya elimu inayoendelea ndani ya takribani shule saba zinazozunguka kata hiyo.
Hata hivyo kamati hiyo kupitia ziara yake ya kukagua na kupokea taarifa ya miradi mbalimbali na maendeleo ya Shule za Msingi na Sekondari ya Mandewa ilimwagiza Mwenyekiti wa Maendeleo ya Kata, Baraza la Ardhi la Kata, Kamati za Shule na Watendaji ngazi ya vijiji na vitongoji kushughulikia haraka kero sugu hususani ya utambuzi wa ardhi na mipaka baina ya maeneo ya shule kadhaa na makazi ya wananchi.
Akiongoza ziara ya kamati hiyo jana kutembelea shule za Msingi Mwaja, Unyakumi, Unyinga, Unyankhae, Mughenyi, Manguanjuki na Sekondari pekee ya Mandewa zilizopo ndani ya kata hiyo, Mwenyekiti wa (CCM) Kata ya Mandewa Hamis Haji Ireme, pamoja na mambo mengine, alionesha kutoridhishwa na mgogoro wa muda mrefu wa mwingiliano wa mipaka baina ya eneo la shule ya Unyinga na makazi ya watu.
“Naagiza watendaji wote wanaohusika kaeni kikao cha haraka na wahusika wote kumaliza changamoto ya mgogoro huu wa ardhi kwa kwa ustawi na mustakabali mzuri wa maendeleo ya taaluma ndani ya Kata ya Mandewa…lakini hata kero hii ya watoto kukosa maji kwenye baadhi ya shule kama pale shule ya msingi Mwaja ni suala dogo tu la kuyavuta umbali wa takribani mita mia moja tu sijui tunakwama wapi?,” alihoji Ireme.
Pia Ireme alionesha kuchukizwa na hatua ya kusuasua kwa ujenzi wa vyoo vya shule ya Sekondari Mandewa maarufu vyoo vya TASAF vilivyovunjwa na moja ya makampuni ya upimaji ramani maeneo kwa lengo kupitisha barabara kwenye eneo hilo jambo ambalo mpaka sasa hakuna kinachoendelea zaidi ya kutelekeza mashimo matupu na kampuni hiyo kutokomea kusikojulikana.
Aidha, kamati hiyo ilikumbana na kero nyingine ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama kwenye mashule, umeme, upungufu wa madarasa, madawati, matundu ya vyoo na kubwa zaidi suala la takribani shule zote kutokuwa na hati miliki ya maeneo-changamoto ambazo kama juhudi za makusudi za kumaliza hazitafanyika huenda zikaleta athari kwa maendeleo ya elimu ndani ya kata hiyo inayoongoza kuwa na eneo kubwa miongoni wa kata zote ndani ya Mkoa wa Singida.
Kwa upande wake, Katibu wa (CCM) wa Kata hiyo Comrade Yusuph Makera maarufu ‘Kijanga’ alisema ziara hiyo ya Chama Cha Mapinduzi kubwa imelenga kusikiliza kero na kuchagiza kasi ya maendeleo kwenye miundombinu ya miradi mbalimbali ya kitaaluma-na kwamba chama hakitasita kuchukua hatua kali kwa wahusika watakaopuuzia maagizo na maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo ya siasa.
Kijanga aliomba serikali kupitia Baraza la Madiwani na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa namna ya pekee kuitazama Kata ya Mandewa kama ‘icon’ na kuipa kipaumbele kibajeti kwenye mipango mbalimbali ya kimkakati kwa kuzingatia jiografia yake, uzalishaji, sanjari na ongezeko kubwa la watu wanaohamia kila kukicha…jambo linalohitaji uwepo wa huduma zote muhimu za kijamii.
Akizungumzia kero zilizoibuliwa baada ya ziara hiyo Kijanga alisema tayari kamati ya siasa imetoa maelekezo ya namna bora ya kukabiliana na kero hizo, ikiwemo ile ya mwamko duni wa wazazi katika kuchangia maendeleo ya shule sanjari na kilio cha muda mrefu cha kukosa ruzuku toka serikalini kwa Shule ya Msingi Mughenyi.
Pia alisema mgogoro unaohusisha Shule ya Msingi Unyankhae juu ya kudaiwa fidia kutoka wamiliki wa eneo hilo, na changamoto ya ukosefu wa jengo la utawala ndani ya Shule ya Sekondari Mandewa na kupelekea mpaka sasa walimu kuendelea kutumia madarasa kwa shughuli za utawala ni miongoni mwa mambo yanayoendelea kushughulikiwa.
“Tunaomba wananchi wetu waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake sikivu chini ya Rais Samia Suluhu..tayari tumepeana maelekezo ya namna bora ya kumaliza kero zilizojitokeza kupitia ziara hii na kila kitu kitakwenda sawasawa,” alisema Kijanga.
Social Plugin