Daktari Bingwa wa Magonjwa ya akili wa Hospitali ya Taifa ya magonjwa ya Akili -Mirembe Dodoma Dkt. Innocent Mwombeki.
NA DOTTO KWILASA,DODOMA.
Kutokana na hali hiyo amewataka akina mama kuacha matumizi ya vilevi wanapokuwa wajawazito ili kuwanusuru watoto walio tumboni kuzaliwa wakiwa na matatizo ya afya ya akili.
Dkt. Mwombeki ameyasema hayo jijini Dodoma katika maadhimisho ya siku ya Afya ya Akili Duniani yaliyoenda sambamba na hamasa ya mapambano dhidi ya unywaji wa pombe kupita kiasi ambapo amesema mama mjamzito anaweza kuwa chanzo cha kusababisha mtoto aliye tumboni kuzaliwa akiwa na matatizo ya afya ya akili.
"Ustawi wa mwenendo wa kitabia na uwezo wa kiakili kwa watoto ni msingi mzuri,lazima kuwaandalia kinga dhidi ya magonjwa ya akili katika kipindi cha utu uzima,matatizo hayo humsababishia athari katika ukuaji wa ubongo kwa awapo tumboni,"ameeleza na kuongeza;
"Tunapoangalia ongezeko la watu wenye matatizo ya afya ya akili,lazima tuangalie tangu mtoto anapokuwa tumboni,wapo akina mama wengi wanatumia vilevi wanapokuwa wajawazito,hii ina athari kwa mtoto aliye tumboni.”amesema Dkt. Mwombeki.
Dkt. Mwombeki ametaja sababu nyingine inayosababisha matatizo ya afya ya akili ni pamoja na mtoto kutolishwa vizuri tangu anapozaliwa,kufanyiwa ukatili mbalimbali ,vipigo kwa watoto na manyanyaso mbalimbali.
“Kuna wale ambao wana vinasaba vya matatizo hayo katika ukoo,akipata changamoto kidogo tu katika maisha anajikuta anapata matatizo ya afya ya akili,lakini umasikini ,matatizo kazini yote hayo huchangia mtu kupata matatizo ya afya ya akili,"amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Shedrack Makubi amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha watanzania milioni 7 wana matatizo ya afya ya akili .
"Mkoa wa Dar es salaam ni kinara kwa kuwa na watu wengi wenye matatizo ya afya ya akili kutokana na watu wengi matatizo hayo kwenda Jijini humo kwa ajili ya kupatiwa matibabu,"amefafanua.
Naye Katibu wa Mtandao wa mashirika ya kupambana na matumizi mabaya ya pombe Tanzania (TAAnet) Gladness Munuo mesema ili jamii iwe salama kwa kupunguza wagonjwa ya afya ya akili ni busara kwa serikali kuongeza gharama za vinywaji vikali ili watu wanywe kistaarabu.
Amesema,TAAnet kwa kushirikiana na wanachama wake itaendelea kukumbusha Taifa madhara yanayotokana na unywaji pombe na kuinua kiwango cha maisha ya watanzania kiafya,kijamii na kiuchumi.
Licha ya hayo ameongeza kuwa sheria zilizopo bado zinapuuzwa kwa kiasi kikubwa hali inayopelekea watu kuendelea kuendesha biashara ya pombe bila kufuata sheria bila kujali madhara yatokanayo na pombe.
"Ili uchumi ukue,watu wake wanapaswa kuwa na afya ya akili yenye utulivu,tunataka kuona vijana wetu wanakunywa kistaarabu na kuepuka msongo wa mawazo,tunaamini pombe ikinunuliwa kwa gharama ya juu baadhi ya watumiaji watashindwa kumudu gharama na watakiwa waoga wa kutumia kinywaji hicho na shughuli za kiuchumi zitastawi,hata watoto wetu wadogo wanaoleweshwa pombe watastawi,"amesema.
Amesema , wao kama wadau wa kupambana na madhara ya unywaji pombe uliopitiliza wangependa kuona watunga sera wanalitafutia tatizo hili ufumbuzi kwa kuwa na ubunifu ambao utaokoa maisha, kama vile kutokomeza athari zitokanazo na pombe na unywaji pombe kupindukia.
Wakati haya yakiendelea ikumbukwe kuwa maadhimisho ya siku ya afya ya akili yanafikia leo kilele ambapo kitaifa yamefanyika Jijini Dodoma huku wadau mbalimbali wa afya wakiwa na matumaini kuwa jamii itaendelea kupambana na viashiria vyote vinavyosababisha magonjwa ya akili.
Siku Hii pamoja na mambo mengine imelenga kuijengea jamii uwezo wa utambuzi na ufahamu wa madhara yatokanayo na matumizi ya pombe kupita kiasi pamoja na kuweka nguvu ya pamoja katika harakati za udhibiti wamatumizi mabaya ya pombe Duniani na ndani ya Taifa.
Hata hivyo wadau wa afya ya akili huitumia siku hii kuikumbusha serikali umuhimu wa ufuatiliaji masuala ya visababishi vya magonjwa ya akili kama pombe ,usambazaji na matumizi yake ikiwa ni pamoja na kuongeza uelewa kwa watumiaji pombe kuwataka kutumia pombe kwa kiasi kisicho na athari za Kiafya, uchumi na kijamii bila kubugudhi jamii.
Social Plugin