Mkuu wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mhe. Aziza Mangosongo akizungumza na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walipowasili wilayani humo kwa ajili ya kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mhe. Aziza Mangosongo akizungumza na timu ya maofisa (Hawapo pichani) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walipowasili wilayani humo kwa ajili ya kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Godfrey Kumwembe akiangalia ripoti ya mashine ya EFD (Z- Report) wakati alipomtembelea mfanyabiashara wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma akiwa kwenye kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. George Haule akimuelimisha mfanyabiashara wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Chama Siriwa akisikiliza maoni ya mfanyabiashara wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi inayoendelea mkoani humo. (PICHA ZOTE NA TRA).
****************************
Na Mwandishi wetu
Mbinga
Wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wamekumbushwa kulipa kodi kwa wakati kwasababu kodi hiyo hurudi kwao kupitia miundombinu na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Mhe. Aziza Mangosongo wakati akizungumza na timu ya maofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Makao Makuu Dar es Salaam walipowasili wilayani humo kwa ajili ya kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mlango kwa mlango.
Mkuu huyo wa Wilaya ameeleza kuwa, kodi hulipwa na watu wote wakiwemo watumishi wa serikali na wa sekta binafsi, wakulima, wafugaji, wavuvi pamoja na wafanyabishara, tofauti ni kwamba, kodi inayolipwa na watumishi hukatwa moja kwa moja kupitia mishahara yao.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwahamasisha na kuwakumbusha wafanyabiashara na wananchi wote kulipa kodi kwa wakati ili kuinua uchumi wa nchi yetu na tuondoe ile kasumba ya kusema kwamba watumishi wa serikali hawalipi kodi, watumishi tunakatwa kodi moja kwa moja kupitia mishahara yetu, alisema Mhe. Mangosongo.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka wananchi kuwafichua watu wanaokwepa kulipa kodi kwa kutoa taarifa sahihi za wahusika hao katika maeneo mbalimbali ili washughulikiwe.
“Pia, nawaomba tusisite kuwataja watu wote wanaokwepa kulipa kodi na tujitahidi kutoa taarifa sahihi za wakwepa kodi katika maeneo yetu kwa maana kodi ni afya na ni uhai wetu, aliongeza Mhe. Mangosongo.
Naye, Meneja wa Huduma kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Bi. Honester Ndunguru awali akiitambulisha timu ya maofisa wanaofanya kampeni hiyo alisema kwamba, TRA imejipanga kufikia idadi kubwa ya wafanyabiashara hapa nchini kwa ajili ya kuwaelimisha kuhusu haki na wajibu wao katika suala zima la ulipaji kodi.
“Sisi kama TRA, tumejipanga kufika maeneo mbalimbali kuhakikisha tunawaelimisha walipakodi wetu kujua haki na wajibu wao na leo tumekuja hapa Mbinga kwa lengo hilohilo la kuhakikisha tunawafikishia elimu ya kodi wafanyabiashara wa wilaya hii, alisema Bi. Ndunguru.
Timu ya maofisa wanaofanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani Ruvuma wako wilayani Mbinga wakiendelea kutoa elimu ya kodi na baada ya wilaya hiyo wataelekea Wilaya za Nyasa, Namtumbo na Tunduru.
Social Plugin