Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapha Siyani amejitoa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kupanga njama za ugaidi inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake watatu.
Ametangaza kujitoa leo Jumatano, tarehe 20 Oktoba 2021, dakika chache kupita tangu alipomaliza kutoa uamuzi wa mapingamizi mawili yaliyowekwa na upande wa utetezi kwenye kesi ndogo ndani ya kesi kubwa.
Mapingamizi hayo yalihusu maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo Adam Kasekwa, yasitumike mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri na maelezo hayo yalitolewa baada ya Kasekwa kuteswa.
Katika uamuzi wake, Jaji Kiongozi Siyani amesema, kulikuwa na sababu ya msingi ya kutolewa nje ya saa 4 kwa mujibu wa sheria na kuhusu kuteswa upande wa utetezi haujathibitisha hilo.
Akitangaza kujitoa, Jaji Kiongozi Siyani amesema, kesi hiyo ikiwa itakwenda mfululizo itawachukuwa takribani miezi minne na kwa kuwa yeye kwa sasa ana majukumu, ameona ajitoe aje Jaji mwingine haraka iwezekanavyo.
Baada ya kueleza hayo, Jaji Kiongozi Siyani ameahirisha kesi hiyo hadi Msajili wa Mahakama Kuu atakapompangia jaji mwingine na watuhumiwa wamerejeshwa rumande katika gereza la Ukonga.