JUISI ZA APPLE CERES ZILIZOPO NCHINI NI SALAMA-TBS



Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Bw.Lazaro Msasalaga akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam. 

****************** 

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilipokea taarifa kutoka mtandao wa kimataifa wa Mamlaka za Udhibiti Usalama wa Chakula uliopo chini ya FAO na WHO kuhusu uwepo sumukuvu aina ya patulin kwenye juisi ya apple ceres kwenye matoleo ya Juni 14 hadi 30 2021 hivyo wakaamua kujiridhisha na kugundua juisi zilizopo sokoni za apple ceres ni salama. 

Ameyasema hayo leo Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Bw. Lazaro Msasalaga wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza katika mkutano huo, Bw.Msasalaga amesema mara baada ya kupokea taarifa hiyo kwenye mtandao wa INFOSAN walichukua hatua za kufuatilia taarifa za uwepo wa matoleo hayo ya juisi na kumtembelea wakala wa msindikaji aliyepo Dar es Salaam na kukagua nyaraka za juisi zilizoingizwa kipindi cha nyuma na juisi zilizopo kwenye ghala. 

"Baada ya ufuatiliaji huo kwa kina TBS ilibaini kuwa matoleo ya juisi za tufaa ( apple ceres juice) ya mwezi Juni , 2021 hayajaingia nchini na tutaendelea kuhakikisha hayatoingia nchini". Amesema Bw.Msasalaga. 

Aidha amesema wataendelea kulinda usalama na ubora wa bidhaa zote wakati wote zilizopo nchini na zinazoingia nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post