KIWANDA CHA KUZALISHA MIPIRA YA MIKONO KUANZA UTENDAJI NOVEMBA


 Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
BOHARI ya Dawa (MSD) iko mbioni kuanza uzalishaji wa mipira ya mikono (gloves) katika kiwanda kipya kilichopo Idofi mkoani Njombe kinachotegemewa kufunguliwa mnamo mwezi Novemba mwaka huu 2021.
 
Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi Mkuu Bohari ya Dawa, Meja Jenerali Gabriel Mhidze (Dkt) wakati akizungumza na Maafisa Habari wa Idara ya Habari - MAELEZO hivi karibuni kuhusu maboresho yaliyofanywa na taasisi hiyo katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya unakuwa endelevu na wa uhakika.
 
Meja Jenerali Mhidze ameeleza kuwa mwishoni mwa mwezi Agosti 2021 Bunge lilipitisha Muswada wa Sheria, ambapo sheria inayoendesha MSD imebadilishwa na kuiwezesha MSD kuzalisha bidhaa za afya ambapo katika majukumu matatu ya msingi ya Bohari ya dawa ya Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji limeongezeka jukumu jingine la kuzalisha dawa na vifaa tiba.
 
“Tumeona mipira ya mikono inatumika sana katika hospitali zetu kwa kufanyia upasuaji hata shughuli nyingine za matibabu, tukaamua kununua kiwanda cha uzalishaji wa mipira ya mikono ambacho kitakuwa kiwanda cha kwanza cha kuzalisha bidhaa hiyo kwa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika. Tunategemea kiwanda hicho kitazalisha jozi za mipira 240,000 ndani ya saa 24”. Alisema Meja Jenerali Mhidze.
 
Amefafanua kuwa mpaka sasa viwanda viwili vya MSD tayari vimeanza uzalishaji, ambavyo ni pamoja na Keko Phamathetical Industry, ambacho serikali imeipa MSD jukumu la kukisimamia pamoja na kiwanda cha Barakoa ambavyo vyote vipo Keko Dar es Salaam.

MSD inategemea kuongeza viwanda vingine vinne ambavyo vinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Novemba.
Amevitaja viwanda vingine ambavyo vinategemewa kuanza uzalishaji hivi karibuni ni kiwanda cha dawa ya ngozi ikiwa ni pamoja na mafuta maalum kwa ajili ya wenye ulemavu wa ngozi, dawa, vidonge, dawa za maji na kapsuli.

Gharama zitakazookolewa kwa mwaka kwa bidhaa za afya zitakazozalishwa katika viwanda hivyo ni shilingi bilioni 33.2 ukilinganisha na kiasi cha shilingi bilioni 54.5 zinazotumika kununua kwa washitiri kwa mwaka.

Kiwanda cha Keko ambacho MSD imepewa jukumu la kukisimamia kimeweza kuongezewa uwezo wa uzalishaji kutoka uzalishaji wa dawa aina moja hadi kufikia dawa aina 10 katika kipindi cha mwaka mmoja Julai, 2020 hadi Mei, 2021.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post