MAJALIWA: RAIS SAMIA AMETOA SH. BILIONI 2.46 UKARABATI VITUO VYA MIZANI NCHINI
Tuesday, October 05, 2021
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa bilioni 2.469 kwa ajili ya kuvifanyia maboresho vituo 42 vya mizani nchini kikiwemo na kituo cha Mingoyo kilichopo eneo la Mnazi Mmoja kwenye barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi mkoani Lindi.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa muda wa miezi miwili kuanzia leo Oktoba 5, 2021 hadi Novemba 30, 2021 uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi uwe umetenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mabasi na maegesho ya malori.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 5, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Mnazi Mmoja mkoani Lindi baada ya kukagua kituo cha Mizani cha Mingoyo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imetenga bajeti katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kufunga Load Cells za kisasa (electronic Load Cells) katika vituo vyote 42 vya mizani nchni.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kumuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Lindi, Mhandisi Efatha Mlavi akifanyie maboresho kituo cha Mizani cha Mingoyo ili kurahisisha utendaji kazi katika mizani hiyo ikiwemo uingiaji na utokaji wa magari.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa kituo cha mabasi cha Mnazi Mmoja Waziri Mkuu amesema eneo hilo linakuwa kwa kasi na linahitaji liwe na kituo cha mabasi pamoja na kituo cha kuegeshea malori ili kupunguza msongamano uliopo sasa. “
Baada ya Waziri Mkuu kutoa agizo hilo wakazi wa Mnazi Mmoja waliishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia kwa kuwajali na kwamba wanaahidi kuendelea kuiunga mkono.
Kadhalika, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya maradi wa ujenzi wa barabara ya Hingawali-Navanga (km 14.1) na Navanga-Pangabuhi (km 8), Mkoani Lindi inayojengwa kwa kiwango cha changarawe ambao ujenzi wake umefikia asilimia 40.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ambayo inajengwa kwa gharama ya shilingi milioni 299.9 utakuwa mkombozi kwa wananchi wa maeneo hayo kwa kuwa utarahisisha usafirishaji.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin