Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS AITAKA WIZARA YA NISHATI KUHAKIKISHA MRADI WA BWAWA LA NYERERE UNAKAMILIKA KWA WAKATI

 


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameitaka wizara ya Nishati kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mradi wa kufua umeme katika Bwawa la Julius Nyerere unakamilika kwa wakati.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme katika Bwawa la Julius Nyerere ambapo amesema ni muhimu wizara ya Nishati kupitia shirika la umeme nchini (Tanesco) kuimarisha usimamizi, kuongeza wataalam sehemu zenye upungufu pamoja na kuongeza umeme utakaoendesha vema mitambo ya mkandarasi  wakati huu wa ujenzi wa mradi .

Aidha  Makamu wa Rais ameagiza Wizara ya Nishati, Tanesco pamoja na Mkandarasi kupitia upya mpango kazi wa ujenzi wa mradi huo pamoja na kuongeza vitendea kazi na muda wwa kufanya kazi ili  kuepusha kucheleweshwa kwa mradi.

Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha kwa wakati ambapo mpaka sasa jumla ya shiling trioni 2.8 zimelipwa kulingana na mkataba. Makamu wa Rais amewapongeza wasimamizi wa mradi huo kampuni ya kitanzania ya TECU kwa kuendelea kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa watanzania pamoja na kutumia malighafi za Tanzania katika ujenzi wa mradi huo.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kulinda mradi huo wakati wote ili kuepusha hujuma zinazoweza kujitokeza wakati na baada ya ujenzi. Pia amewaagiza viongozi wa mikoa kuchukua hatua kali kudhibiti idadi ya mifugo iliopo na inayoingizwa katika Bonde la mto Rufiji pamoja na kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa bonde hilo kwa manufaa ya mradi.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati January Makamba amesema maelekezo yote yaliotolewa na Makamu wa Rais, Wizara itaanza kuyafanyia kazi mara moja na  kwamba Wizara itasimamia  kwa ukamilifu dhamana iliopewa katika ujenzi wa mradi huo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com