*******************************
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ametembelea shule ya Sekondari Mungaa ili kujionea namna serikali ya awamu ya sita ilivyoboresha miundombinu kupitia Shilingi Milioni 30 zilizotolewa shuleni hapo.Akizungumza na walimu na wanafunzi wa shule hiyo,Mtaturu ameahidi kutoa Shilingi 100,000 kwa mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza katika mtihani wa kidato cha nne. “Hii sio kwa wanafunzi tu bali kwa walimu watakaosaidia kupatikana daraja la kwanza 10 nitampatia Shilingi Milioni 1,lengo la kufanya hivi ni kutoa hamasa kwa vijana na walimu wao kuweza kuweka bidii kwenye maandalizi ya kujiandaa na mitihani ya Taifa wa mwaka huu,”alisema Mtaturu.
Aidha ,amekabidhi Compyuta 5 ,mashine moja ya printa ili kusaidia wanafunzi kujifunza masuala ya TEHAMA,vifaa vya michezo kwa wanafunzi na sukari kilo 25 kwa ajili ya walimu wakiwa shuleni iwasaidie kupata chai na kuahidi kupeleka kilo 100 za mchele kwa ajili ya kambi ya wanafunzi wa kidato cha nne.
Akikabidhi vitu hivyo Mtaturu amewaasa walimu hao kutunza vifaa vilivyotolewa ili vinufaishe jumuiya ya shule na jamii kwa ujumla.
“Sasa hivi tupo kwenye maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia hivyo matumizi ya TEHAMA hayakwepeki na ndio maana tangu nimeingia bungeni nimeshasaidia kompyuta katika shule ya Sekondari Dkt Shein Misughaa na leo nakabidhi hapa Mungaa,”alisema.
Amesema hiyo itawasaidia walimu kufanya marejeo kwenye kwenye ufundishaji wa masomo mbalimbali kupitia mtandao na hivyo kuwa nyenzo muhimu ya kupandisha taaluma.
“Naomba wazazi wenzangu tushirikiane na walimu katika kukuza taalum shuleni,tubebe jukumu hili na kuliona ni letu sote,niwapongeze walimu kwa jitihada zenu kubwa katika kuwafundisha watoto wetu bila ya kuchoka,niwaahidi tu serikali yetu ni sikivu itaendelea kuangalia stahiki zenu kila mara ili kuwapa motisha zaidi,”alisisitiza.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mungaa Gabriel Dulle ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha za kujenga miundombinu shuleni.
Social Plugin