MIFUGO NA UVUVI WASHINDI WA PILI MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA DUNIANI.



Mgeni Rasmi wa kilele cha Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda (kulia) akimkabidhi zawadi ya kombe, Afisa Utumishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Scholastica Mdoe baada ya Wizara hiyo kuibuka mshindi wa jumla wa nafasi ya pili kwenye kipengele cha Taasisi zilizoonesha ubunifu wa teknolojia mbalimbali wakati wote wa Maadhimisho hayo yaliyohitimishwa  (17.10.2021) Mkoani Kilimanjaro.

Viongozi, Watumishi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na wadau wake wakifurahia kwenye picha ya pamoja muda mfupi baada ya kukabidhiwa zawadi ya kombe na cheti baada ya kuibuka washindi wa jumla wa nafasi ya pili kwenye kipengele cha Taasisi zilizoonesha ubunifu wa teknolojia mbalimbali wakati wote wa Maadhimisho hayo yaliyohitimishwa (17.10.2021) Mkoani Kilimanjaro

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeibuka mshindi wa pili kwenye matokeo ya jumla ya Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya chakula Duniani kwa mwaka huu yaliyotangazwa wakati wa kilele cha Maadhimisho hayo  (17.10.2021) mkoani Kilimajaro.

Wizara imeshika nafasi hiyo kufuatia kuongoza kwenye kipengele cha Taasisi iliyoonesha ubunifu wa kuchakata mazao yake kwenye mabanda ya maonesho kwa taasisi zote zilizoshiriki kwenye maadhimisho hayo ambapo nafasi ya kwanza imechukuliwa na banda la Umoja wa mataifa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa zawadi ya kombe na cheti kufuatia ushindi huo, Mkurugenzi Msaidizi huduma za Ugani (Mifugo) Dkt. Kejeri Gillah amesema kuwa ushindi huo umetokana na umoja na mshikamano uliopo baina ya Wizara, Taasisi na wadau waliopo chini yao ambapo amesisitiza kudumisha ushirikiano huo wakati wote.

“Tulikuwa na wadau wa tasnia ya maziwa, nyama, ufugaji wa kuku na wale wanaojihusisha na ufugaji wa samaki na ulinzi wa rasilimali za uvuvi kwa ujumla, hawa wote walikuwa wakionesha ubunifu wa namna gani wanahakikisha mlaji anapata lishe yenye mazao yote yanayotokana na sekta za mifugo na uvuvi na kwa kweli watu wamefurahia huduma zetu mara zote walipofika hapa” Amesema Dkt. Gillah.

“Niendelee kuwasisitiza wananchi waendelee kula vyakula ambavyo vina asili ya nyama kwa sababu vimethibitika kutoa protini namba moja ambayo inaimarisha afya ya mwili na akili ya mlaji na waongeze kiwango cha unywaji wa maziwa ili wawe na nguvu na uwezo wao wa kufikiria uongezeke pia” Amesisitiza Dkt. Gillah.

Kwa upande wake mmoja wadau walioonesha ubunifu katika banda la Wizara hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Kiwanda cha Maziwa cha Nronga kilichopo Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Bi. Hellen Usiri ameishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Bodi ya Maziwa nchini (TDB) kwa ushirikiano mkubwa wanaowapa wakati wote wanapowahitaji.

“Niiombe Wizara iendelee kuweka msisitizo kwenye huu mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa sababu utasaidia sana kuinua kiwango cha ufaulu hapa nchini kwa sababu tayari tumeshaona matokeo yake kwenye shule ambazo zimeshaanza kutekeleza mpango huu” Amesema Usiri.

Awali akisoma hotuba ya kufunga Maadhimisho hayo kwa mwaka huu, Mgeni rasmi ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Prof. Adolph Mkenda amesema kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia taasisi yake ya Wakala ya Maabara ya Veterinari nchini (TVLA) imeweza kuzalisha dozi milioni 63 za chanjo kwa ajili ya kuikinga mifugo dhidi ya magonjwa ya mdondo, kimeta, chambavu, Homa ya mapafu ya ng’ombe na Ugonjwa wa kutupa mimba ambapo pia ameongeza kuwa Taasisi hiyo inaendelea kufanya utafiti ili kuzalisha chanjo za magonjwa mengine yanayoathiri mifugo hapa nchini.

“Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi, Wizara hiyo ina mpango wa kufanya ujenzi wa mitambo ya barafu, kutengeneza chanja za kukaushia dagaa,ununuzi wa vifaa vya kukaushia samaki vinavyotumia mwanga wa jua na ujenzi wa soko kubwa la samaki la Kipumbwi wilayani Pangani mkoani Tanga” Amesema Prof. Mkenda.

Maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka huu yalianza Oktoba 10 hadi leo ambapo wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wamepata fursa ya kujifunza teknolojia mbalimbali za uchakati wa mazao mbalimbali ya sekta za kilimo, mifugo na Uvuvi huku pia wakipata elimu inayohusu lishe bora.

 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post