OLE SABAYA ANYOLEWA, AFIKISHWA MAHAKAMANI KESI YA UHUJUMU UCHUMI


Ikiwa ni siku tatu tangu alipohukumiwa kwenda jela miaka 30, yeye na wenzake wawili kwa makosa ya nunyang’anyi wa kutumia silaha, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amefikishwa tena mahakami leo Jumatatu, Oktoba 18, 2021 kusikiliza kesi yake nyingine ya uhujumu uchumi.

Sabaya amefikishwa mahakamani hapo na wenzake akiwa amenyolewa kipara kama ambavyo wafungwa huwa wananyolewa kwa mujibu wa taratibu za magereza.

Shahidi wa nne upande wa Jamhuri katika kesi ya Uhujumu Uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Philemon Kazibila (64) ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuwa, vijana wawili kati ya wanne waliokuwa na mtuhumiwa huyo walijitambulisha kuwa ni maofisa usalama wa Taifa wanaoshughulikia ukusanyaji wa kodi.

Kazibila amedai hayo Jumatatu ya Oktoba 18,2021 mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Patricia Kisinda wakati akitoa ushahidi.

Shahidi huyo ambaye ni karani katika kampuni ya Mrosso Injector Pump inayomilikiwa na mfanyabiashara Francis Mrosso, amesema kuwa vijana hao walitangulia kuingia ofisini kwake kumuuliza kama wanalipa kodi kabla ya Sabaya kuingia ofisini humo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Ofmed Mtenga, shahidi huyo alidai kuwa kabla Sabaya na vijana wake kufika ofisini hapo, Januari 22,2021 mmoja wao alikwenda kwenye ofisi hiyo na kupatiwa huduma ambapo alishindwa kupewa risiti kutokana na mashine kutokuwa na mtandao.

Alimtaja mtu huyo aliyefika ofisini hapo siku hiyo Watson Mwahomange na kupewa huduma ya pump.

Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa baada ya Sabaya kufika ofisini hapo alitakiwa kutoka nje ya ofisi hiyo ambapo baada ya muda waliondoka na Mrosso, ambaye baadaye alimpigia simu (Kazibila) na kumtaka ampatie bodaboda kadi ya benki ya CRDB.

Alidai mahakamani hapo kuwa baada ya kumpa dereva huyo kadi ya benki, jioni bosi wake (Mrosso) alirejea akiwa na huzuni na hakujua kitu gani kimemkuta.

Katika hatua nyingine shahidi huyo aliwatambua na kuwashika bega mtuhumiwa wa kwanza (Sabaya) na mtuhumiwa huyo wa tatu kwenye kesi hiyo, Mwahomange, ambapo alidai aliwaona katika eneo hilo.

Katika shauri hilo la uhujumu namba 27,2021 washitakiwa wengine ni Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post