Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Prof. Mchome: Wanaotumia Kesi Za Ubakaji Kama Kitega Uchumi Wachukuliwe Hatua

 Na Mwandishi  Maalum, Kigoma
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria,Profesa  Sifuni Mchome amesisitiza kwamba, ni kosa la  jinai kwa mtu yeyote  kumsingizia  mtu mwingine tuhuma za ubakaji au unyanyasaji wa kijinsia  kwa madhumuni ya kujipatia fedha.

Ametoa maelekezo hayo siku ya  jumatano wakati wa Kikao Kazi na  Kamati zinazoshughulikia   mapambano ya  kupinga vitendo vya ukatili wa jinsia (MTAKUWWA),  baada ya kuelezwa kwamba, kuna baadhi ya wazazi   katika Mkoa wa Kigoma ambao wamekuwa wakitengeneza  kesi za ubakaji  kama  vitega uchumi.

“Niwaombe sana,   mzazi au  mlezi ambaye atabainika kuwa  ametumia njia za uongo kutengeneza  tuhuma za ubakaji na kisha kujipatia fedha, huyo  anafanya jinai na anapashwa kuchukuliwa sheria kama mhalifu yeyote yule muanze kufanya hivyo.” akasisitiza Katibu Mkuu.

Maelekezo  ya Katibu Mkuu Mchome, yalitokana na  taarifa  za kuwapo kwa baadhi ya wazazi ambao wamekuwa wakitengeneza matukio ya  ubakaji na kasha  kuamua kuyamaliza kifamili  na kujipatia fedha.

WP Sakina  Rashid Ndauka ambaye  anasimamia Dawati la Jinsia  la Polisi Kigoma Ujiji, alieleza Kikao Kazi hicho kwamba,  sababu za  mashauri mengi ya  ubakaji kutokamilika ni kutokana na  wazazi wawalalamikaji kuamua kumaliza kifamilia.

 Akasema  katika mashauri 56 yakiwamo ya  ubakaji, ulawiti na mimba za utotoni, ni mashauri 12 tu yaliyoweza kukamilika  huku  watuhumiwa wawili wakihukumuwa kifungo cha miaka 30 jela.

Hata hivyo Afisa Dawati huyo akasema  kuna baadhi ya  wazazi ambao wamegeuza   matukio ya ubakaji  kama kitega uchumi na kujipatia fedha.

 Akatoa mfano kwamba kuna kesi moja ya  tuhuma za ubakaji  aliyokuwa anaifuatilia,  lakini katika mahojiano na  Bint aliyetuhumiwa kubakwa,  bint yule aliomba  azungumze na afisa dawati bila ya wazazi wake kuwapo.

“ Binti yule aliomba azungumze nami bila ya wazazi wake, na ndiyo alipokiri kwamba yeye hajabakwa isipokuwa wazazi wake wameitengeneza kesi hiyo kwa kumfundisha kwamba achukue boda boda kwenda mahali  Fulani na kisha wao  hutengeneza  mazingira kwamba boda boda yule amembaka na kumfikisha polisi” akaeleza WP Sakina Ndauka.

Akaongeza kwamba shauri   alipotaka  shauri lile kulifanyia  uchunguzi zaidi na hatimaye kulifikisha mahakani, wazazi wa bint yule waliomba wakalimalize wao wenyewe na huko ndipo wanapokweda kuchukua  fedha.

WP Sakina amesema  ameshakutana na  mashauri  hayo ya kuwambambikia  tuhuma za ubakaji  kama  mara mbili hivi.

 Akaongeza kwamba,  licha ya  familia nyingi  kuamua kumaliza kifamilia  matukio ya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia lakini pia kimekuwapo na visa vya walalamikaji kuwakana watuhumiwa au mashahidi kukataa kutoa ushahidi na hivyo kuleta ugumu wa ukamilishaji wa mashauri hayo kwa wakati  na hivyo kujikuta na mlundikano wa majalada.

Kufuatia hali hiyo  hasa ya  utengenezaji wa kesi za ubakaji, ndipo  Katibu Mkuu  Profesa Sifuni Mchome alipotaka wadau wa haki jinai kuanza  kuwachukulia hatua wazazi watakaobainika kutengeneza kesi hizo.

Katika hatua nyingine,  Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Christopher Kadio amewasihi wazee kutimiza wajibu wao kwa kutoa taarifa  kuhusu   matukio  yasiyo ya kawaida yanayoendelea katika  jamii zao.

 Amema wazee wa nchi hii  bado wanasauti  na wanapaswa kuzipaza sauti hizo dhidi ya maovu yanayoendelea katika jamii.

Katibu Mkuu Kadio akabainisha kwamba kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia  sababu kubwa inayotolewa ni mmonyoko wa maadili katika jamii  kuwa mkubwa  sana .

“ Mmomonyoko wa maadili katika  jamii ni mkubwa sana,   kumetokea nini? Na nyinyi wazee mpo, lakini si kwa wazee wetu tu, kila mmoja wetu ajitafakari na kuchukua  hatua” akahimiza Katibu Mkuu  Mambo ya Ndani.

Pia akasema  serikali inaendelea  na mchakato wa kuhakikisha kuwa Polisi Jamii inashuka mpaka  ngazi ya  Kata. Lakini akasema huduma hiyo  haitakuwa na faida  ikiwa jamii   hazitatoa ushirikiano ili kupunguza uhalifu na ukatili katika jamii.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com