Rais Samia Suluhu Hassan, amuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu, kutoa Sh. bilioni moja kabla ya Novemba 30, mwaka huu, kwa ajili ya kuchangia ujenzi unaoendelea wa hospitali ya Wilaya ya Arusha.
Aidha, amekabidhi hundi ya Sh. bilioni 1.39 kwa vikundi 152 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyopo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Rais Samia alitoa agizo hilo Oktoba 17, 2021, baada ya kuzindua hosptali hiyo ya kisasa ambayo ujenzi wake umegharimu zaidi ya sh. bilioni 2.5 ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
“Nimefurahishwa sana kwa jinsi ambavyo mmekusanya vizuri mapato yenu ya ndani na kujenga hospitali hii ya kisasa. Kwa sababu hii, nimemwagiza waziri wa TAMISEMI, Ummy, kuleta hapa kiasi cha sh. bilioni moja kwa ajili ya kuunga mkono ujenzi huu ambao tayari wana majengo mawili ya kisasa yaliyokamailika,” alisema.
Rais Samia alisema licha ya kutoa fedha hizo, pia serikali kuu itatoa dawa na vifaatiba katika hospitali hiyo, ili wanachi waendelee kupata huduma bora za afya.
Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwaomba wananchi kuendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya Jiji la Arusha na maendeleo yao, huku akiwataka watumishi kuendelea kukusanya mapato ya jiji hilo kwa uadilifu.
Kwa upande wake, Waziri Ummy alimshukuru Rais Samia kwa kufungua hospitali hiyo na kuahidi kuzitoa fedha hizo kabla ya Juni 30, mwaka huu kama alivyoagiza.