Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Evariste Ndayishimiye, anatarajiwa kuwasili nchini kwa ziara ya Kitaifa ya siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Oktoba, 2021.
Akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amesema Mhe. Rais Ndayishimiye atawasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma tarehe 22 Oktoba na kuelekea Ikulu ya Chamwino ambako atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Waziri Mulamula amesema baada ya kuwasili Ikulu ya Chamwino, Rais Ndayishimiye atakagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21 kwa heshima yake na baadae viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha na kufuatiwa na mazungumzo rasmi.
Balozi Mulamula amesema akiwa jijini Dodoma tarehe 22 Oktoba mchana, Mhe.Rais Ndayishimiye atatembelea na kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kuzalisha mbolea ya asili yenye mchanganyiko wa madini ya phosphate na samadi kinachojengwa katika eneo la viwanda la Nala, kiwanda ambacho kinajengwa na Wawekezaji wa kampuni ya Itracom Fertilizers Limited (ITRACOM) kutoka nchini Burundi na baadaye jioni atahudhuria dhifa ya kitaifa itakayofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Balozi Mulamula ameongeza kuwa tarehe 23 Oktoba 2021 Mhe. Rais Ndayishimiye ataelekea Zanzibar ambako atapokelewa na Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kuwa na mazungumzo na mwenyeji wake huyo na baadaye ataelelekea Mkoani Dar es Salaam ambapo ataungana na mwenyeji wake Mhe. Rais Samia .
Amesema akiwa jijini Dar es Salaam Rais Ndayishimiye anatarajiwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukagua ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaoendelea nchini kutokea stesheni ya Dar es salaam hadi stesheni ya Kwala - Ruvu pamoja na kutembelea bandari kavu ya Kwala inayojengwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania katika eneo hilo la Kwala mkoani Pwani ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa bandari kavu hiyo.
Akizungumzia ziara hiyo ya Rais Ndayishimiye nchini, Balozi Mulamula amesema ni mwendelezo wa hatua zinazochukuliwa na Serikali za Tanzania na Burundi za kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwa maslahi ya pande zote na itaendeleza na kukuza ushirikiano uliopo na kufungua fursa ya kuanzisha maeneo mingine ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuwawezesha Waheshimiwa Marais hao (wa Tanzania na Burundi) kufahamu hatua zilizofikiwa katika kutekeleza maagizo yao waliyoyatoa wakati wa ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Burundi tarehe 16 na 17 Julai, 2021.
Balozi Mulamula amesema Mhe. Rais Ndayishimiye na ujumbe wake wanatarajiwa kuondoka nchini kurejea Burundi tarehe 24 Oktoba 2021 baada ya kumaliza ziara yake.