Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya, akifungua Semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji (hawapo pichani), kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika mkoani Nj
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Njombe, Mhandisi Ruth Shalluah akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya (hayupo pichani), kufungua Semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji (hawapo pichani), kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika mkoani Njombe
Baadhi ya washiriki wa semina ya mafunzo ya Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 wakimsikiliza mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Njombe (hayupo pichani), wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika mkoani Njombe
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya, (aliyeketi katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa semina ya mafunzo kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 kwa wadau wa usafirishaji, inayofanyika mkoani Njombe.
Wakili Msomi Fanueli Muhoza kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), akitoa elimu kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 kwa wadau wa usafirishaji mkoa wa Njombe.
PICHA NA WUU
............................................
Mkuu wa mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya, amewataka wadau wa usafirishaji mkoani humo kuzilinda barabara nchini kwa kubeba uzito stahiki kwenye magari yao ili waweze kuwa wasafirishaji wenye tija.
Ameyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo kwa wadau wa usafirishaji kuhusu Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 inayofanyika kwa siku moja mkoani humo.
“Ndugu washiriki, mtakubaliana nami kuwa kama tunataka kuwa wasafirishaji wenye tija na ufanisi, ni lazima tuwe na barabara nzuri, barabara ambazo ni bora zinapunguza gharama za uendeshaji, gharama za vipuri, lakini vile vile zinapunguza muda wa safari na hivyo kuongeza kiasi cha faida ambacho msafirishaji anatarajia kukipata”, amesema Mhandisi Rubirya.
Ameongeza kuwa Serikali inatumia fedha nyingi katika ujenzi wa barabara nchini lakini vile vile kwenye matengenezo yake ili ziweze kuwa katika hali nzuri, hivyo ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kwa kuona umuhimu wa kuandaa mafunzo hayo ili kujenga uelewa kwa wasafirishaji wanaofanya makosa kutokana na kukosa uelewa wa sheria hiyo.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Meneja wa TANROADS mkoa wa Njombe Mhandisi Ruth Shalluah, amesema kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa utoaji elimu ya Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 ambayo imekuwa ikitolewa kwa wadau wa usafiri wa barabara nchini tangu mwaka 2018 kabla ya kuanza kutumika rasmi mwezi Machi mwaka 2019.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa mafunzo haya yanalenga kuongeza uelewa wa pamoja baina ya wasafirishaji na Serikali ambao ndio wa simamizi wa sheria hii, na hivyo mafunzo haya yanatolewa pia kwa watumishi wa mizani ili waweze kutoa huduma ya upimaji uzito wa magari kwa ufanisi” amesema Mhandisi Shallua.
Kwa upande wake Mhandisi Leonard Saukwa ambae ni Msimamizi wa Mizani kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), amewaambia waandishi wa habari kuwa mbali na utoaji wa elimu kuhusu sheria hiyo ya udhibiti uzito wa magari, semina hiyo pia imelenga kuelimisha namna ya upatikanaji wa vibali kwa wasafirishaji wa mizigo maalumu.
Mafunzo ya Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018 yamepangwa kufanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Morogoro, Dodoma, Njombe, Mbeya, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Geita, Tabora, Mwanza, Arusha na Tanga, ambapo hadi kufikia sasa tayari, wadau wa usafirishaji katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara Morogoro na Dodoma wamenufaika na mafunzo hayo.
Social Plugin