Asasi za kiraia (Azaki) zimetakiwa kufanya kazi kwa weledi,uadilifu,uzalendo kwa maslahi mapana ya taifa ikiwa ni pamoja na kutumia tafiti na takwimu vizuri ambazo zitasaidia kutoa majawabu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya watanzania.
Wito huo umetolewa leo jijini Dodoma na Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai wakati wa ufunguzi wa wiki ya AZAKI (2021) ambapo amesema asasi hizo hazina budi kutafuta fedha ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuleta tija na vipaumbele vya taifa .
Ndugai amezitaka asasi hizo kuwa na mwenendo wa kukosoa viongozi wa serikali lakini pia wana wajibu wa kuwapongeza hasa pale wanapofanya vizuri wanapotekelza majukumu yao kwa ajili ya maslahi ya watanzania wote.
Kwa upande wake rais wa Taasisi ya uwezeshaji asasi za kiraia [Foundation For Civil Societt- FCS] Dkt,Stigmata Tenga amesema ipo haja kwa bunge kuleta mabadiliko na kupitia upya sheria ,taratibu na miongozo ambayo inaziongoza asasi hizo ili ziweze kushiriki vyema katika kutekeleza kazi zao na majukumu yao kwa maendeleo ya taifa.
Maonyesho ya wiki ya azaki kwa mwaka (2021) yanakwenda sambamba na kauli mbiu isemayo Azaki na Maendeleo.