TANZANIA YATUMIA BILIONI 362 KUHIMILI ATHARI MABADILIKO YA TABIANCHI
Monday, October 11, 2021
Na Ahmed Sagaff - MAELEZO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeanza kutumia kiasi cha shilingi bilioni 362 zilizotengwa kwenye mwaka wa fedha 2021/2022 kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo alipokuwa akitoa msimamo wa Tanzania kwenye majadiliano ya mkutano wa 26 wa nchi wananchama wa mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
“Miradi hiyo inatekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, nishati, misitu, viwanda na TEHAMA pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi,” ameeleza Mhe. Jafo.
Amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zimeilazimu Serikali ya Tanzania kutumia asilimia mbili mpaka tatu ya Pato la Taifa katika kukabiliana na madhara hayo.
“Fedha hizi ni nyingi sana ukizingatia hali ya uchumi wa Tanzania na vipaumbele vya Serikali katika kuleta maendeleo kwa watu,” amebainisha Waziri Jafo.
Msimamo wa Tanzania
Pamoja na hayo, waziri huyo amesema miongoni mwa vipengele saba vinavyounda msimamo wa Serikali ya Tanzania ni kuzitaka nchi zilizoendelea kutoa Dola za Marekani bilioni 100 kila mwaka kwa mataifa yanayoendelea kama ilivyoainishwa kwenye Mkataba wa Paris uliopitishwa mwaka 2015.
Mhe. Jafo amehabarisha kwamba Tanzania inazitaka nchi zilizoendelea kuzijengea uwezo nchi zinazoendelea ili ziweze kupunguza uzalishaji wa gesijoto duniani, kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapatiwa teknolojia kwa gharama nafuu na kwa uwazi, na kutokijumuisha kilimo miongoni mwa sekta zinazotakiwa kupunguza gesijoto.
“Mkutano huu ufikie maamuzi yatakayowezesha upatikanaji wa fedha za kuwezesha nchi zinazoendelea kutekeleza michango yao na kwamba mapitio ya michango hiyo yafanyike kila baada ya miaka mitano,” amefahamisha Mhe. Jafo.
Aidha, amedokeza kuwa Tanzania inahimiza utekelezaji wa program ya miaka mitano kuhusu jinsia na mabadiliko ya tabianchi.
“Suala la upunguzaji wa gesijoto kwenye uso wa dunia halina budi kufanyika ili ongezeko la joto liwe chini ya nyuzi joto mbili, aidha juhudi za ziada zinahitajika ili ongezeko lisivuke nyuzi joto 1.5 kwa ajili ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Makubaliano ya Paris kwenye kipengele cha sita yanatoa fursa ya nchi mbalimbali kushirikiana kwenye upunguzaji wa gesijoto kwa kutumia mbinu ya biashara.
“Msimamo wa Tanzania ni kwamba nchi inayouza ziada ya upunguzaji isijumuishe kiwango kilichouzwa kwenye orodha yake ya upunguzaji ili kusitokee kuhesabiwa mara mbili kwani nchi iliyonunua ziada hiyo ndiyo itaweka kiwango hicho kwenye orodha yake ya upunguzaji gesijoto,” amebainisha Waziri Jafo.
Tangu alipoingia madarakani Machi 2021, Rais Samia amekuwa akiitekeleza Ibara ya 235 ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 ambayo inaielekeza Serikali kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari zitokanazo na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin