Kaimu Mkuu Kitengo cha uandaaji wa Viwango vya Huduma TBS, Bw.Henry Msuya akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Shirika la Viwango Tanzania TBS leo Jijini Dar es Salaam.
Afisa Viwango TBS, Bw.Bakari Hassan akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Shirika la Viwango Tanzania TBS leo Jijini Dar es Salaam.
***********************
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa Viwango katika Sekta ya Utalii ili kuhakikisha kuwa huduma za Utalii zinazotolewa hapa nchini zinaendelea kuwa zenye ubora katika kila eneo na hivyo kuwa kivutio kikubwa kutokana na huduma bora zinazokidhi viwango.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam, Afisa Viwango TBS, Bw.Bakari Hassan amesema kuandaa viwango katika sekta hiyo kutaongeza thamani kwenye maeneo mbalimbali ya huduma za utalii pia kujenga na kuendelea kukuza taswira ya nchi ya kuwa na vivutio vyenye ubora Duniani.
"TBS itaendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wa sekta hii ili kufanana au kuwazidi wenzetu kimataifa na pia kushirikiana na wadau wa sekta hii kuandaa viwango hivyo". Amesema Bw.Hassan.
Aidha amesema TBS kwa kuona umuhimu wa sekta ya utalii mnamo mwaka 2017 ilianzisha kamati ya kitaalamu ya kuandaa viwango katika sekta hiyo.
"Kamati hii imeundwa na wadau kutoka taasisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Wizara ya Utalii,Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Usafiri wa anga Tanzania (TCAA), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Maktaba ya Taifa ya Utalii (NMT), Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TATO), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT)". Amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu Kitengo cha uandaaji wa Viwango vya Huduma TBS, Bw.Henry Msuya amesema TBS inawakaribisha wadau wote wa sekta ya utalii kushirikiana pamoja kudumisha viwango ili kuendeleza huduma bora zinazotolewa kwenye sekta hiyo kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii na kuongeza pato la taifa na hivyo kukuza uchumi wa nchi yetu.
Social Plugin