Tembo
Na Dinna Maningo,MWANZA
IMEELEZWA kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu,mifugo na shughuli za kilimo katika maeneo ya hifadhi za Wanyamapori nchini kumechangia kupungua kwa Tembo huku vifo na uharibifu wa mazao vikiongezeka.
Pia jumla ya migogoro 41,404 imeripotiwa kwa kipindi cha mwaka 2012-2019 na kati ya hiyo migogoro 29,798 imeripotiwa katika maeneo ya shoroba kati ya 2017-2020, huku vifo vya Binadamu 2012-2020 ni 1,173.
Majeraha ya kudumu kwa binadamu 2012-2020 ni 204,Majeraha ya muda kwa Binadamu 2012-2020 ni 514,vifo vya wanyama kwa mwaka 2012-2020 ni 1,146,Uharibifu wa mazao 2012-2020 ni ekari 51,330.
Hayo yamebainika wakati wa mafunzo ya uandishi wa habari za Sayansi,Teknolojia na Ubunifu kwa Watafiti na Waandishi wa habari kutoka mkoa wa Kagera,Mwanza na Mara yaliotolewa na Tume ya Taifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu (COSTECH) katika ukumbi wa mikutano Ofisi ya mkuu wa mkoa Mwanza.
Jarida la Julai,2021 lililoandaliwa na Dkt. Cecilia Leweri na Jerome Kimaro lililowasilishwa katika Tume hiyo ya Taifa linaeleza kuwa kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) zinaonyesha kuwa binadamu wameongezeka zaidi huku tembo wakizidi kupungua.
Utafiti huo unaeleza kuwa miaka ya 1970-1990 idadi ya watu ilikuwa takribani milioni 30 na idadi ya tembo ilikuwa 300,000 ,hadi kufikia 2020 idadi ya watu ni milioni 60 wakati idadi ya tembo ni takribani 60,000 hali inayoonyesha ongezeko la idadi ya Tembo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya watu.
Jarida hilo linaeleza kuwa sababu za kupungua kwa tembo linatokana na migogoro ya Binadamu na Wanyamapori inayohusishwa na mabadiliko ya idadi ya watu,shughuli za kiuchumi,hali ya hewa,mifumo ya matumizi ya ardhi na mabadiliko ya kiteknolojia.
Tafiti za TAWIRI zinaonyesha kuwa nchini Tanzania migogoro hiyo imekuwa suala kubwa katika jamii likichochewa zaidi na ongezeko kubwa la idadi ya watu lililosababisha kuongezeka kwa mahitaji ya matumizi ya maliasili na kusabisha hasara za kijamii,kiuchumi, kibioanuwi na hivyo kuathiri uhifadhi wa Wanyamapori.
Hali hiyo inaelezwa kusababisha kupanuka kwa miji na shughuli za binadamu kama kilimo,ufugaji,uwindaji wa wanyamapori katika maeneo ya makazi ya wanyamapori hususani shoroba,maeneo ya mtawanyiko na maeneo ya kinga(Bafa).
Kwa mujibu wa utafiti huo unaeleza kuwa shoroba ambazo zipo katika hali ya kupotea ni pamoja na ushoroba kati ya Hifadhi ya Gombe na Pori la Akiba la Masito-Ugalla kupitia hifadhi ya Misitu ya Uvinza.
Zingine ni Mfumo wa Ikolojia wa Ruaha-Rungwa na Tarangire kwenda Pori la Akiba la Swagaswaga lililopo katikati ya Tanzana,Mfumo wa Ikolojia wa Udzungwa na Pori la Akiba la Selous kwa upande wa kusini mwa Tanzania na Hifadhi ya Jamii ya Wami-Mbiki na eneo la Pori la Handeni (GCA) kwa upande wa Mashiriki mwa Tanzania.
Tafiti zinaeleza kuwa kuingiliwa kwa makazi ya wanyamapori pamoja na shoroba kunatishia uhusiano wa kiikolojia wa maeneo yaliyohifadhiwa (PAs) na kwamba ushahidi wa kiutafiti unaonyesha kuwa,kuna shoroba za Wanyamapori ambazo bado zinafaa kwa matumizi ya wanyamapori.
Utafiti huo umebaini kuwa kuwepo kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori ikiwemo ya ardhi imechangia kutokea kwa vifo kati ya watu na wanyamapori na uharibifu wa mazao.
Utafiti wa TAWIRI unaonyesha kuwa vifo vya wanyama kwa mwaka 2012/2013 ni 46, 2013/2014 vifo 93,2014/2015 ni 107,2015/2016 vifo 64,2016/2017 ni 130,2017/2018 ni 149, 2018/2019 ni vifo 203, 2019/2020 vifo 354.
Vifo vya binadamu kwa mwaka 2012/2013 ni 69, 2013/2014 ni 61, 2014/2015 vifo 59,2015/2016 ni 102, 2016/2017 ni 132, 2017/2018 vifo 380, 2018/2019 ni 266 na 2019/2020 vifo ni 104.
Utafiti unaonyesha kuwa majeraha ya kudumu kwa binadamu mwaka 2012/2013 ni 23, 2013/2014 majeraha 31, 2014/2015 ni 20, 2015/2016 ni 20, 2016/2017 ni 30, 2017/2018 ni 20, 2018/2019 walikuwa 60 na 2019/2020 ni 0 hakukuwa na binadamu mwenye majeraha ya kudumu.
Majeraha ya muda kwa binadamu 2012/2013 ni 38,2013/2014 ni 49, 2014/2015 majeraha 41, 2015/2016 ni 78, 2016/2017 ni 54, 2017/2018 majeraha 29, 2018/2019 ni 149, 2019/2020 waliokuwa 76.
Utafuti huo unaonyesha kuwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori imesababisha uharibifu wa mazao ambapo 2012/2013 ekari 1,518 ziliharibiwa,2013/2014 ekari 4,046, 2014/2015 ni 6,786, 2015/2016 ni 8,924, 2016/2017 ekari 4,567, 2017/2018 ni 5,016, 2018/2019 ekari 10,547 na 2019/2020 zilikuwa ekali 9,926.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo ya utafiti imependekeza kuoaniasha sera za sekta zinazohusika na matumizi ya ardhi kama vile Sera ya ardhi,wanyamapori,misitu,maji,kilimo,mifugo,na mazingira,pamoja na kuhakikisha kuwa shoroba za wanyamapori zinajumuishwa katika mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji,Wilaya,Mkoa na Taifa.
Pendekezo lingine ni kurasimisha shughuli mbadala za kiuchumi zinazoendana na uhifadhi wa Wanyamapori mbali na shughuli za kilimo,shughuli hizo ndiyo ziwe pekee zitakazofanyika katika maeneo yaliyo karibu na makazi ama mapitio ya wanyamapori ambazo ni pamoja na ufugaji wa nyuki na utalii wa maeneo ya asili na utalii wa kitamaduni.
Pia kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za uhifadhi,kuwashirikisha wataalamu wa afya kufahamu takwimu za majeraha yaliyosababishwa na wanyamapori,watunga sera,na wadau mbalimbali wawe mstari wa mbele kuunga mkono utekelezaji wa mkakati wa kitaifa nakupunguza migogoro kati ya Binadamu na wanyamapori na urejeshaji wa shoroba.
Social Plugin