Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UHURU KENYATTA NA JOE BIDEN WA MAREKANI KUKUTANA KWA MARA YA KWANZA IKULU WHITE HOUSE


Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta anatarajiwa kukutana na mwenyeji wake, Joe Biden wa Marekani kwenye Ikulu ya White House, kujadialiana kuhusu masuala mbalimbali.

Rais Kenyatta anakuwa rais wa kwanza wa Afrika kukutana na kiongozi huyo wa Marekani, na Ikulu ya Marekani imesema marais hao wawili watazungumzia namna ya kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Kenya, lakini pia umuhimu wa uwazi kuhusu mifumo ya fedha kitaifa na kimataifa.

Ajenda ya mkutano huo imewekwa wazi, saa chache kabla ya mkutano huo na hii inakuja baada ya uchunguzi wa nyaraka za Pandora kubaini kuwa Familia ya rais Kenyatta amehifadhi mali za siri zenye thamani ya Dola Milioni 30.

Marais hao wawili pia watazungumzia kuhusu juhudi za kulinda na kuheshimu demokrasia na haki za binadamu kwenye ukanda wa pembe ya Afrika hasa Ethiopia, namna ya kuimarisha uchumi na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi.

Biden na Kenyatta pia wanatarajiwa kujadiliana kuhusu uamuzi wa Mahakama ya haki ya Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa eneo la Bahari na Somalia.

Baada ya mkutano huu rais Kenyatta anatarajiwa kumaliza ziara yake nchini Marekani, alikokwenda kuongoza kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambacho kwa mwezi Oktoba nchi hiyo ya Afrika Mashariki ndio Mwenyekiti.

 

-RFI



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com