KAMATI ZA KUTOKOMEZA UKATILI TARIME ZAJENGEWA UWEZO ILI KUTOA TAARIFA SAHIHI ZA UKATILI



Na Frankius Cleophace Tarime.

 Kamati za Mpango Mkakati wa Taifa wa  Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia  kwa wanawake na watoto  (MTAKUWWA)zimeendelea kijengewa uwezo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ili ziendelee kutoa taarifa sahihi juu ya Ukatili.

Kamati zilizojengewa uwezo ni kutoka kata za Manga na Kiore katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime Peter Mwita kutoka kituo cha  Maendeleo ya kilimo na ushari Mogabiri kupitia Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tarime ambao wanatekeleza mradi wa kutokomeza ukatili, alisema kuwa lengo la kujengea uwezo kamati hizo ni kuweka mikakati na mipango ya pamoja ili kulinda haki za mama na mtoto pamoja na kutoa taarifa kwa wakati juu ya wahanga wa ukatili.

“Mafunzo haya tumeyatoa kwa baadhi ya wanafunzi, Waratibu elimu kata, Watu wenye ulemavu,Viongozi wa dini,Walimu wakuu katika shule za msingi ambao ni wawakilishi na watu hawa ndiyo wanaunda kamati za Mtakuwwa na elimu waliypewa kupitia Afisa Ustawi, Msaidizi wa kisheria na Mtu wa Dawati la Polisi itasaidia kuibua majanga yanayokumba wanawake na watoto katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime”, alisema Peter.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wilaya ya Tarime Mkoani Mara Bony Matto ambaye pia alikuwa mkufunzi alisisitiza  suala la Utoaji wa taarifa kwa wakati juu ya wahanga wa ukatili wa kijinsia ili waweze kusaidiwa.

“Matukio ya ukatili kwa Tarime ni mengi lakini jamii haipo tayari kutoa taarifa sasa kamati hii ya MTAKUWWA itasaidia kutoa taarifa kwa wakati mfano Tarime kuna ndoa za utoto wazazi wanaozesha mabinti wao ili kaka zao waweze kupata fedha za kulipa mahali ili nao waweze kuoa jambo ambalo ni ukatili”, alisema Matto.

Aidha Washiriki wa mafunzo hayo ambayo yamezikutanisha kamati za MTAKUWWA walisema kuwa suala la umaskini linatajwa kuchangia ukatili wa kijinsia kwenye jamii ambapo wameiomba serikali kuendelea kuimarisha uchumi wa kaya ili kupunguza ukatili kwenye jamii.

 Vile vile Washiriki hao waliongeza kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waone uhimu wa kuboresha Dawati la Jinsia na Watoto kwa kujenga vituo vya kuhudumia wahanga wa ukatili nje ya vituo vya polisi ili kutoa huduma stahiki.

 “Wananchi wengi wanaogopa Polisi endapo kituo cha polisi kitajengwa nje ya majengo ya polisi itasaidia kupata taarifa nyingi kupitia wahanga wa ukatili pamoja na mashaidi”, alisema Waitara Kemo mmoja wa washiriki .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post