Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Baadhi ya Wamiliki na wafanyakazi wa vituo vya kuoshea Magari 'Car Wash' Mjini Shinyanga wamelalamika kufungiwa vituo vyao ghafla bila ya kupewa maelekezo yoyote huku wakipewa siku 5 hadi siku ya Jumatatu, wawe wameshafika kwenye Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kupewa utaratibu wa Serikali.
Wakizungumza na Malunde 1 blog (Majina yao yamehifadhiwa) wamesema Oktoba 12,2021 waliambiwa kwa njia ya mdomo kufunga vituo hivyo hadi siku ya Jumatatu na Afisa Mipango Miji wa Manispaa ya Shinyanga aliyefika katika vituo vyao.
"Wamiliki vituo vya Car wash tunaonewa ,tulipewa leseni halali kwa ajili ya kuendesha hii kazi lakini leo tunafungiwa eti hatuna kibali cha mkurugenzi wa Manispaa...Swali Je? tulipoomba leseni hapakuwa na maelekezo hayo? iweje watufungie wakati tuna leseni hai",wamesema.
"Car wash zimefungwa mjini Shinyanga leo (14.10.2021) ni siku ya
tatu, Car wash zimefungwa bila kuambiwa sababu tena ghafla, wote hadi wenye leseni wameambiwa
tufunge...vijana wanalia kukosa ajira,wenye magari,pikipiki wamekosa sehemu za
kuoshea magari yao",wameeleza
Kufuatia kufungwa kwa baadhi ya vituo vya kuoshea Magari (Car wash) Mjini Shinyanga imesababisha watu kukosa huduma za kuosha magari na pikipiki zao huku vijana waliojiri kupitia kazi ya kuosha magari wakiwa katika wakati mgumu kwa kukosa pesa ili kuhudumia familia zao.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura amesema wamefunga vituo vya kuoshea magari kwa sababu ya wamiliki wa vituo hivyo kutofuata taratibu za serikali na kuweka vituo hivyo holela na kuharibu mipango mji.
Amesema walifanya Oparesheni ya kukagua vituo vyote vya kuoshea magari katika Manispaa ya Shinyanga na kubaini wamiliki wake hawakufuata utaratibu wa Serikali kwa kupewa vibali na Afisa Mipango Miji, bali wameingia mikataba na wamiliki wa maeneo kitendo ambacho ni kinyume na utaratibu na kulazimika kuvifunga.
“Manispaa ya Shinyanga tuna mpango wa kuutengeneza Mji kuwa hadhi ya Jiji, hivyo kutokana na kuwepo kwa vituo vingi vya kuoshea magari holela, bila ya kupata vibali kutoka Halmashauri kwa Afisa Mipango Miji nikaagiza wavifunge vyote na kufuata utaratibu. Wafike Halmashauri wapewe utaratibu,”amesema Satura.
Amesema hawajafunga vituo hivyo vya kuoshea magari kwa maksudi kwa sababu wanafahamu vimetoa ajira nyingi kwa vijana, bali wanachotaka ni kufuatwa kwa utaratibu wa Serikali juu ya mipango miji, kwa kupata kibali na kuonyeshwa maeneo sahihi ya shughuli hizo, na siyo kuweka kila mahali na kuharibu Mji.
Social Plugin