WAFANYABIASHARA RUVUMA WAIPONGEZA TRA KUENDESHA KAMPENI ELIMU KWA MLIPAKODI

Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. James Ntalika akimpatia zawadi Mfanyabiashara wa Mjini Songea mkoani Ruvuma baada ya kumuelimisha masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mliapakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Chama Siriwa akimsikiliza mfanyabiashara wa mjini Songea mkoani Ruvuma alipokuwa akitoa maoni yake wakati wa kampeni ya elimu kwa mliapakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Godfrey Kumwembe akimuelimisha mfanyabiashara wa eneo la Peramio mjini Songea mkoani Ruvuma wakati wa kampeni ya elimu kwa mliapakodi inayoendelea mkoani humo.
Afisa Msimamizi wa Kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Shaga Gagunda akimuelimisha mfanyabiashara wa mkoani Ruvuma wakati wa kampeni ya elimu kwa mliapakodi inayoendelea mkoani humo. (PICHA ZOTE NA TRA).

*******************************

Na Mwandishi wetu

Ruvuma

Wafanyabiashara wa mjini Songea mkoani Ruvuma wameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkoani humo ambapo wamesema kwamba, kwa sasa kuna mabadiliko makubwa ndani ya mamlaka hiyo ikilinganishwa na hapo awali.

Wakizungumza wakati wa kampeni hiyo inayoendelea mkoani humo, wafanyabiashara hao wameeleza kuwa, licha ya TRA kuwafikia na kuwapatia elimu ya kodi, kuna maboresho makubwa yamefanyika kwenye mifumo ya ulipaji kodi suala ambalo limeondoa usumbufu kwa walipakodi.

“Mwanzoni mfanyabiashara alikuwa akichelewa kulipa kodi, TRA walikuwa wanakuja na kufunga maduka lakini kwa sasa wameboresha mifumo yao kiasi kwamba tunakumbushwa kwa meseji kwenye simu zetu za mkononi na bado wanatufuata kutupatia elimu, na kutukumbusha kulipa kodi kwa wakati, kwakweli TRA wanastahili pongezi, alisema Bw. Chasiko Mhagama, mfanyabiashara wa Mjini Songea.

Naye, mfanyabishara wa kufua nguo kwa kutumia mashine Bi Advera Katabaruki wa mkoani Ruvuma ameeleza kuwa, kampeni ya elimu kwa mlipakodi imesadia kuwajulisha mambo mengi waliyokuwa hawayajui kwa mfano utunzaji wa kumbukumbu za biashara, matumizi sahihi ya mashine za EFD pamoja na umuhimu wa kulipa kodi.

“Kampeni hii ya elimu kwa mlipakodi imetufunza mambo mengi sana ambayo tulikuwa hatuyajui kama vile jinsi ya kutunza kumbukumbu zetu za biashara, kutoa risiti sahihi za EFD kwa wateja wetu na sisi kudai risiti tunapokwenda kununua bidhaa kwa wafanyabiashara wakubwa ikiwa ni pamoja na kutukumbusha kulipa kodi kwa wakati, alisema Katabaruki.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa vitambaa Bw. Klasa Chengula amefurahia elimu aliyoipata na kuipongeza TRA kwa kubadilika tofauti na zamani ambapo walikuwa wanawaogopa maofisa wa mamlaka hiyo kwa kutokuwa na ukaribu na walipakodi wao.

“Kiukweli maofisa wa TRA wamejirekebisha sana tofauti na mara ya kwanza ambapo ilikuwa ukipigiwa simu unaitwa TRA tulikuwa tunapata mawazo kweli lakini hivi sasa TRA haigopeki na wamekuwa marafiki kiasi kwamba wamepita kutupa elimu nzuri ya kodi wala hatujajificha wala kufunga maduka, alisema Chengula.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi mkaoni Ruvuma inaendelea kufanyika katika maeneo mbalimba ya mkoani humo ambapo walipakodi wanaelimishwa juu ya haki na wajibu wao, utunzaji wa kumbukumbu za biashara, umuhimu wa kulipa kodi kwa wakati pamoja na kutoa risiti stahiki za EFD kila wanapouza bidhaa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post