WAKUU WA WILAYA WATAKIWA KUELIMISHA WANANCHI KUHUSU UHIFADHI


Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) akizungumza na watendaji wa Mkoa wa Geita kuhusu kuelimisha wananchi suala la uhifadhi katika kikao cha Kamati ya Mawaziri 8 kilichofanyika Mkoani Geita leo. Kushoto ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki na Kulia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi.


Baadhi ya watendaji wa Mkoa wa Geita wakimsikiliza wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hayupo pichani) katika kikao cha Kamati ya Mawaziri 8 kilichofanyika Mkoani Geita leo.


Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ludovick Nduhiye akitambulisha Mawaziri katika kikao cha Kamati ya Mawaziri 8 kilichofanyika Mkoani Geita leo.

***************************

Wakuu wa Wilaya nchini wametakiwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa uhifadhi na kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokuwa akizungumza na watendaji wa Mkoa wa Geita katika kikao cha Kamati Mawaziri 8 wa Kisekta kilichofanyika Mkoani Geita leo.

“Tunaomba Wakuu wa Wilaya mtusaidie kuelimisha wananchi faida na hasara za uhifadhi ili mwananchi anapoingia kwenye hifadhi ajue ametenda kosa kama mhalifu mwingine ” Mhe. Masanja amesisitiza.

Mhe. Masanja amewasihi Wakuu wa Wilaya kutoa ushirikiano katika kusimamia hifadhi.

“Wahifadhi wana changamoto kubwa sana kwa sababu wananchi hawaogopi kuingia maeneo ya hifadhi, hivyo bila kusaidiwa na Wakuu wa Wilaya Hifadhi hizi zinaenda kufa” Mhe. Masanja ameongeza.

Aidha, Mhe. Masanja ameweka bayana kuwa endapo mwananchi atakamatwa na mifugo hifadhini, ahakikishe anaandikishiana na mhifadhi idadi ya mifugo aliyonayo kabla ya kuondoka.

“Mwananchi anapoingiza mifugo hifadhini ana tabia ya kukimbia anapomuona askari wa uhifadhi, hivyo kama mwananchi umekamatwa simama toa maelezo andikisha ulichokamatwa nacho ili mnapoenda mahakamani askari atatoa ushahidi kwamba alisaini hapa na ng’ombe niliowakamata ni hawa” Mhe. Masanja amesisitiza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post