WATANZANIA 940,507 WAPOKEA CHANJO YA JANSEN


Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Watanzania 940,507 wamepokea chanjo ya Jansen ikiwa ni asilimia 88.9 ya chanjo zote 1,058,400 za aina hiyo zillizotolewa na Serikali ya Marekani kupitia mpango wa COVAX FACILITY.
 

Hayo yamesemwa leo jijini Mwanza na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa alipokuwa akitoa taarifa ya kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
 

“Shehena ya chanjo 1,065,000 aina ya Sinopharm zilizokuja wiki iliyopita kutoka China zimeanza kusambazwa katika Halmashauri na Mikoa yote nchini na zoezi la uchanjaji linaendelea,” amefahamisha Msigwa.
 

Pamoja na hilo, amehabarisha kuwa Tanzania inatarajia kupokea chanjo zingine aina ya Pfizer dozi 500,000 mwishoni mwa mwezi huu wa kumi kutoka COVAX FACILITY.
 

“Na dozi hizi ni sehemu ya Dozi Milioni 3.7 za chanjo aina ya Pfizer ambazo nchi yetu itazipata kwa awamu kutoka COVAX Facility, tayari hivi navyoongea majokofu ya baridi kali 14 yenye uwezo wa kuhifadhi chanjo zote Milioni 3.7 yameshafungwa pale jijini Dar es Salaam.
 

“Kupitia hii COVAX FACILITY tunatarajia kupata dozi Milioni 11.8 na pia kuna juhudi nyingine za kupata chanjo zinazoendelea ili kutimiza lengo letu la kutoa chanjo kwa asilimia 60 ya Watanzania wote,” ameeleza Msigwa.
 

Sambamba na hayo, amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (UVIKO-19) ambazo ni uvaaji barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni, kuepuka misongamano, kukaa umbali wa meta moja au zaidi, kufanya mazoezi, na kula lishe bora.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post