Mratibu wa masuala la Lishe katika Halmashauri ya Mji wa Tarime Mkoani Mara Monica Ouk
Na Frankius Cleophace - Tarime
Ili kujenga Misingi bora ya ukuaji wa mtoto pamoja na kuboresha suala la Lishe wazazi wameshauriwa kutumia vyema siku elfu moja ikiwa ni pamoja mtoto kunyonya maziwa ya mama kwa muda wa miezi Sita.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa masuala la Lishe katika Halmashauri ya Mji wa Tarime Mkoani Mara Monica Ouk wakati akizungumza kuelekea siku ya Lishe kitaifa ambayo ufanyika kila Oktoba 23 kila mwaka na mwaka huu maadhiomisho yatafanyika Mkoani Tabora kitaifa.
Monica alisema kuwa wazazi mara nyingi wamekuwa wakishindwa kunyonyesha watoto wao kwa kipindi cha Miezi sita kutokana kujikita kwernye majukumu kwa wingi jambo ambalo linaweza kuchangia suala la Udumavu.
Monica alisisitiza jamii kuendelea kufuata kanuni za lishe ili watoto waweze kukuwa na kustawi vizuri ikiwa ni pamoja na kuhudhuria kliniki pale wanapopata ujauzito mpaka wanajifungua.
“Suala la kunyonyesha maziwa ya Mama kwa mtoto ni muhimu sana pia mama anashauriwa kutumia vyakula vinavyopaswa kuboresha motto akiwa tumboni ili kuweza kujenga mtoto”, alisema Monica.
Kauli Mbiu ya Mwaka huu katika kilele cha siku ya Lishe kitaifa inasema kuwa “Lishe Bora ni Kinga Thabiti dhidi ya Magonjwa, Kula Mlo Kamili , Fanya Mazoezi, Kazi Iendelee.
Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa kwa mwaka huu ni ya pili tangu kuanzishwa kwake ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika Mwaka 2020 Mkoani Dodoma, ambapo siku hii imetajwa kutumika kama jukwaa muhimu katika kutekeleza na kuendeleza azma ya Serikali ya kutokomeza aina zote za utapiamlo nchini na kuongeza uelewa na ufahamu juu ya lishe bora na hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa na wananchi ili kuleta mabadiliko chanya hususani katika ngazi ya jamii.