WAZIRI MCHENGERWA AELEKEZA KUWABADILISHIA VITUO VYA KAZI MAAFISA UNUNUZI SERIKALINI
Friday, October 01, 2021
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaelekeza watendaji wa ofisi yake kuwa na utaratibu wa kuwabadilishia vituo vya kazi Maafisa Ununuzi na Ugavi wote waliokaa muda mrefu kwenye kituo kimoja ili kukabiliana na changamoto ya maafisa hao kujihusisha na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi Serikalini.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akifungua kikao kazi cha Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji hao kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.
Mhe. Mchengerwa amesema, wapo Maafisa Ununuzi na Ugavi waliokaa muda mrefu kwenye vituo vya kazi na kuona ofisi ni zao na hatimaye kuanza kufanya kazi kwa mazoea, hivyo ofisi yake inalazimika kuwa na utaratibu wa kuwahamisha ili kuendelea kusimamia uadilifu mahala pa kazi.
“Hakuna Afisa Ununuzi na Ugavi au mtumishi yeyote wa umma mwenye hati miliki ya kukaa muda mrefu kwenye kituo kimoja cha kazi na kuongeza kuwa, ofisi yake itahakikisha inawajibika kuendelea kulinda maadili ya utendaji kazi kwa watumishi wa kada zote,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Ameongeza kuwa, Maafisa Ununuzi na Ugavi watakaohamishwa wawe tayari kufanya kazi watakapopelekwa kwani ni jukumu la Watumishi wa Umma kuwatumikia wananchi mahala popote.
Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, kitendo cha kuwabadilishia Maafisa hao vituo vya kazi kitasaidia sana kuongeza weledi na uwajibikaji mahala pa kazi.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Emmanuel Shindika amempongeza Mhe. Mchengerwa kwa kutoa maelekezo ya kuwa na utaratibu wa kuwabadilishia vituo vya kazi Maafisa Ununuzi na Ugavi ili waondokane na utendaji kazi wa mazoea unaosababisha wajihusishe na vitendo vya rushwa.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Uchambuzi na Ushauri wa Kazi, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Nolasco Kipanda amesema kwa kuwa takribani asilimia sabini ya matumizi yapo upande wa manunuzi hivyo katika kikao kazi hicho mada ya masuala ya ununuzi na ugavi itawasilishwa ili kujenga uelewa wa pamoja kwa Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali katika eneo hilo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameendelea kukemea vitendo vya rushwa kwa Watumishi wa Umma wa kada mbalimbali ikiwemo ya ununuzi na ugavi.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin