Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza wakati wa
kupokea taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli ya robo mwaka kwa bajeti ya
wizara ya mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo jijini Dodoma, ambapo
Waziri Ndaki amesema utaratibu wa ukusanyaji maduhuli uko wazi lakini
kuna shida ya namna ya ukusanyaji pamoja na fedha nyingine kutojulikana
zinapopelekwa baada ya kukusanywa. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Baadhi
ya washiriki wa kikao cha kupokea taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli ya
robo mwaka kwa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sekta ya Mifugo kwa
mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo jijini Dodoma, wakifuatilia
mwenendo wa kikao hicho kilichoongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki (Mb). (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -
Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Na. Saja Kighumbe
Akizungumza leo (26.10.2021) katika kikao cha kupokea taarifa ya ukusanyaji wa maduhuli ya robo mwaka kwa bajeti ya wizara ya mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo jijini Dodoma, Waziri Ndaki amesema utaratibu wa ukusanyaji maduhuli uko wazi lakini kuna shida ya namna ya ukusanyaji pamoja na fedha nyingine kutojulikana zinapopelekwa baada ya kukusanywa.
Ameongeza kuwa amesikitishwa na baadhi ya minada ya mifugo, kutofikia malengo yaliyowekwa katika robo ya mwaka ya bajeti kati ya Mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu na kumlazimu kutoa uamuzi wa kuwaondoa baadhi ya wasimamizi wa minada kwenye nafasi zao na wengine kuwaweka katika kipindi cha uangalizi ili kufuatilia utendaji kazi wao katika ukusanyaji wa maduhuli.
“Picha hii tunayoiona hapa inaonyesha tatizo ni kubwa namna ya kukusanya pesa katika ngazi ya chini kwenye vituo vyetu na siyo makao makuu, sababu zinazotajwa na watu wanaokusanya ni zile zile miaka yote na bado tulikusanya, kwa nini kipindi hiki makusanyo yashuke?” amehoji Mhe. Ndaki
Kufuatia ukusanyaji wa kiwango cha chini wa maduhuli katika kipindi cha robo mwaka ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2021/22 Sekta ya Mifugo, Waziri Ndaki ameagiza kufikia tarehe 28 mwezi huu kuwe kumeundwa timu ya ufuatiliaji wa makusanyo ya maduhuli.
Ameongeza kuwa timu hiyo ambayo anataka akutane nayo kabla ya utekelezaji wa majukumu yake, inapaswa kufanya kazi kwa weledi na kutoa taarifa za ukweli bila kupendelea wala kumuonea mtu na kuhakikisha inapita katika minada yote ya mifugo na halmashauri zote nchini kufuatilia utekelezaji wa ukusanyaji wa maduhuli.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amesema amekuwa akikerwa na utoroshaji wa rasilimali za mifugo nchini kwenda nje ya nchi na uingizaji wa mazao ya mifugo kinyume na utaratibu ambapo wanaweza kuwa wanaingiza mazao mbalimbali kwa kuwa hawalipi kodi na kuathiri uzalishaji ndani ya nchi mambo ambayo hayavumiliki.
Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiathiri kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato ya mifugo na mazao yake hali inayoifanya serikali kukosa mapato.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo Bw. Amosy Zephania akizungumza kando ya kikao hicho amesema maazimio yaliyotolewa katika kikao hicho ni kupitia na kufanya tathmini ya kila kituo cha kukusanyia mapato na kupima utekelezaji wa ukusanyaji, kuimarisha timu ya kufuatilia maduhuli sehemu zote katika sekta ya mifugo pamoja na halmashauri kurejesha fedha kutokana na makusanyo kwa ajili ya kuingizwa katika mfuko mkuu wa serikali.
Muda wowote kama ambavyo itaelekezwa na uongozi wa wizara, utaratibu huu wa kukutana kila robo ya mwaka ni maelekezo ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb).
Social Plugin