WIZARA YA AFYA: BILION 4.5 KUBORESHA, KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UVIKO-19 NCHINI
Saturday, October 02, 2021
Na WAMJW – Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi, akiwa amemwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kwenye uzinduzi wa mradi wa Aga Khan Development Network na Aga Khan Health Services, amesema, Serikali kupitia wadau wa Maendeleo inafanya maboresho ya Sekta hiyo kwenye Mikoa 4 ya Dar es Salaam, Mwanza, Lindi na Mtwara kwa Gharama ya Bil. 4.5 kupitia ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya kupitia taasis ya mtandao wa maendeleo ya Aga Khan (AKDN) katika kipindi cha miaka miwili ya mradi.
Dkt. Leonard Subi, akizungumza katika hafla hiyo na uzinduzi wa mradi kwa ujumla ambao ulikwenda sambamba na ukaguzi wa Jengo la uangalizi maalum (‘High Dependence Unit) katika Hospitali ya Amana mkoani Dar es Salaam, amesema jengo hilo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo, ambapo taasisi ya Aga Khan katika hatua za awali tayari imefanikisha kukarabati na kuwekewa vifaa vya kisasa vyenye gharama zinazo fikia takriban Mil. 413 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa uliopo kwenye mikoa 4 hapa nchini.
Dkt. Subi amesema Wizara inaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya UVIKO-19 nchini katika afua za Kinga na Tiba ikiwemo kuimarisha mifumo
“Leo tumekuja kuzindua mradi, lakini tumepata fursa yakukagua jengo kubwa ambalo limekarabatiwa kwa gharama ya shilingi Mil. 176 na kuwekewa vifaa vipya vya kisasa ikiwepo uwekaji wa mfumo wa upatikanaji wa hewa safi ya Oksijeni katika jengo husika, amesema Dkt. Subi na kuongeza kuwa, tayari Serikali imeweka mtambo wa kuzalisha mitungi 200 ya Oksijeni kwa siku katika Hospitali hiyo ya Amana, lakini pia kwenye Hospitali zingine saba za Mikoa.” alisisitiza Dkt. Subi.
Dkt. Subi amesema, kwa sasa wizara inaendelea na utekelezaji mpango wa kuhakikisha Hospitali zote za Rufaa za Kanda, Mikoa, pamoja na baadhi ya Hospitali za Wilaya, zinakuwa na mitambo ya uzalishaji wa Oksijeni hali itakayo saidia kuondosha kabisa tatizo la Oksijeni nchini, huku akionya na kusema lazima watu wafikiri zaidi kinga, kwakuwa kinga ni bora kuliko tiba.
Dkt. Subi ametumia Fursa hiyo, kuwaomba Viongozi wa Dini pamoja na watu wa kada mbali mbali kuendelea kuelimisha makundi yote ndani ya jamii, na kusema, endapo watu wakielimika na kutumia afua ya chanjo itasadia katika mapambano dhidi ya Uviko-19 na hivyo watu watakuwa na afya njema na watawaweza kuendelea na majukumu yao ya ujenzi wa Taifa.
“Mtakumbuka mwezi Aprili, mwaka huu, Mhe. Rais aliunda Kamati ya kutathmini hali ya Uviko-19 nchini, aidha wataalama wetu wakafanya kila wanaloweza hasa katika kuangalia suala la usalama, ufanisi pamoja na ubora wa chanjo, na ndio hiki tunacho kiona sasa, hivyo naomba tuepuke taarifa za upotoshaji hususan zile za kwenye mitandao ya kijamii au kwa watu ambao taaluma zao na uwezo wao bado zina mashaka, taratibu tunazo zitumia ni taratibu za kisayansi lakini zinazo zingatia usalama wa Taifa letu”. Amesema Dkt. Subi.
Dkt. Subi amesema, Serikali imeongeza vituo vya kutolea chanjo ya Uviko-19, kutoka vituo 550 vya awali hadi kufikia 6784 kote nchini, ambapo imesaidia kuongeza mwamko wa watu kuchanja na kuongezeka Idadi yao kufikia watu zaidi ya 460,000 hadi tarehe 29 Septemba 2021.
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin