Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Wizara Ya Kilimo Yasema Serikali Haijazuia Uuzaji Mazao Nje Ya Nchi


Na Mwandishi Wetu,
SERIKALI imesema haijazuia mfanyabiashara yeyote kuuza mazao yake nje ya nchi, na kwamba mkulima wa nchi hii wajibu wake ni kulima , kuvuna ,kuhifadhi na kuuza kwa kuwa hiyo ndio biashara yake.

Akizungumza katika ziara ya kikazi wilayani Mpanda mkoani Katavi baada ya kukagua ,kituo cha kununulia mahindi cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema Serikali haijazuia uuzaji wa mazao nje ya nchi.

“Hivyo kama yupo ambaye amazuiwa kuuza mazao yake nje ya nchi Wizara hiyo inamkaribisha na watampa ushirikiano kwani vibali vyote vya kusafirisha mazao nje ya nchi wanatoa vibali bure ili mradi awe leseni ya kufanya biashara hiyo.

“Serikali imeanza utaratibu wa kujenga na kukodi maghala katika nchi ambazo zina masoko ya mazao kama vile Sudan Kusini, DRC Congo, Kenya, tunaenda kuweka maghala katika nchi hizo ili Bodi yetu ya Mazao Mchanganyiko (CPB) na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) waweke mazao hayo kwenye maghala hayo na kuyauza,”amesema.

Ameongeza wataruhusu wafanyabiashara wa Tanzania waweze kuuza mahindi yao kupitia maghala hayo ili kurahisisha biashara yao.
Kuhusu maombi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko aliyeomba kituo cha Mpanda kuongezwa tani zingine 10,000 kwa ajili ya wakulima kuuza mahindi yao amesema kwa sasa Wizara inapitia vituo vyote ili kujiridhisha na kujua mahitaji kamili ya vituo hivyo.

Amefafanua kwa sababu unaweza kuruhusu wanunue tani hizo kumbe mahindi yenyewe hayapo.“Napita katika kila kituo kujiridhisha na tutafanya ukaguzi huo mpaka Oktoba 15, 2021 ili tukifanya maamuzi tujue kila mkoa utapata mgao wa kiasi gani tutakapowaruhusu kununua mahindi hayo kulingana na kiasi tutakachowaongezea.”

Bashe ameongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amejipambanua kuwalinda wakulima wa Tanzania na wanafahamu bei ya pembejeo imepanda katika soko la dunia hivyo njia pekee ya kumlinda mkulima ni kumpa ruzuku ya mbolea au kununua mahindi yake na hiyo ndiyo sababu Serikali inanunua mahindi ili kulinda wakulima wetu.

Ameongeza mazao mengi ya wakulima yanaathiriwa na uhifadhi hii ni sehemu muhimu sana ndiyo maana serikali inajenga maghala mengi mpaka vijijini ili kuwasaidia wakulima namna ya kuhifadhi mazao kwa ubora lakini pia imekuwa ikitoa elimu sana kwa wakulima namna ya kuhifadhi mazao yao.

“Lakini Serikali inagawa mbegu za kisasa kupitia Taasisi ya Uzalishaji wa mbegu bora ya (ASA) kwa wakulima na imepunguza gharama za mifuko ya kuhifadhia mahindi inayozalishwa na A to Z na kupunguza hasara zinazotokana baada ya kuvuna mazao ambapo mkulima akiingiza mahindi katika mchakato wa kusafisha anapunguza kilo moja kwa kila kilo 100 kwa sababu mahindi yanakuwa na mchanga, mabunzi pamoja na vumbi.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com