Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia (Uvuvi) Dkt. Rashid
Tamatamah (mwenye suti nyeusi), akiwa kwenye zoezi la kukabidhi injini
za kupachika kwenye boti kwa maafisa wafawidhi wa vituo vya ulinzi na
usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria. (Picha na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia (Uvuvi) Dkt. Rashid
Tamatamah, akiwa kwenye picha ya pamoja na watendaji wakuu wa idara
mbalimbali katika Sekta ya Uvuvi wizarani hapo, pamoja na maafisa
wafawidhi wa vituo vitano vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi
Kanda ya Ziwa Victoria. Dkt. Tamatamah amekabidhi injini tano za
kupachika kwenye boti katika vituo hivyo zenye thamani ya jumla ya
Shilingi Mlioni 68.1 (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -
Wizara ya Mifugo na Uvuvi).
Na. Edward Kondela
Serikali
imewataka maafisa wafawidhi waliopo katika vituo vya ulinzi na
usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria, kuhakikisha
wanadhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nchi za jirani pamoja na
kuzuia uvuvi haramu.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema hayo leo
(28.10.2021) katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma,
wakati akikabidhi injini za kupachika kwenye boti zenye uwezo “HP 40”
kwa vituo vitano vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya
Ziwa Victoria.
“Ni matumaini yangu kuwa injini hizi zitakuwa
chachu kwa vituo hivi kufanya kazi kwa weledi pamoja na kusimamia ulinzi
wa rasilimali za uvuvi.” Amesema Dkt. Tamatamah
Aidha,
amesema ili kufikia malengo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kukusanya
maduhuli ya Shilingi Bilioni 40 kwa mwaka wa fedha 2021/22, injini hizo
zitumike katika kuhakikisha vituo husika vinakusanya maduhuli ili
kufikia malengo waliyojiwekea na kufikia malengo makuu ya wizara.
Nao
baadhi ya maafisa wafawidhi waliokabidhiwa injini za boti kwa ajili ya
vituo vyao vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi wamesema
injini hizo zitasaidia kuongeza nguvu katika kudhibiti uvuvi haramu.
Wameongeza
pia injini hizo zitasaidia katika kufuatilia ukusanyaji wa mapato
ambayo ni moja ya mikakati ya wizara na kudhibiti utoroshaji wa mazao ya
uvuvi kwenda nchi za jirani.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia
Idara ya Uvuvi imenunua injini sita za kupachika kwenye boti zenye
thamani ya Shilingi Milioni 68.1 kwa ajili ya kuimarisha Sekta ya Uvuvi
nchini.
Vituo vitano vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za
uvuvi vilivyokabidhiwa injini hizo ni Kanda ya Simiyu na Magu, Kanda ya
Mwanza, Kanda ya Ukerewe, Kanda ya Geita na Kanda ya Marehe Mkoani
Kagera.
Social Plugin