Takriban watu 45 wanahofiwa kufariki dunia baada ya moto kulipuka ndani ya basi Bulgaria.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa nane za usiku kwa saa za Bulgaria karibu na kijiji cha Bosnek, wizara ya mambo ya ndani imenukuliwa ikisema na shirika la habari la BTA.
Watoto walikuwa miongoni mwa waathiriwa wa mkasa huo, afisa wa wizara Nikolai Nikolov ameiambia televisheni binafsi BTV. Watu saba wameripotiwa kuokolewa.
Basi hilo linaaminiwa kuwa lilikuwa linasafiri kutoka Uturuki kuelekea maeneo ya Macedonia Magharibi.
Eneo linalozingira mahali ambapo ajali hiyo ilitokea kwa sasa limefungwa kwa ajili ya uchunguzi wa mkasa huo.
Waziri mkuu wa Macedonia Kaskazini Bw Zoran Zaev tayari amewasiliana na mwenzake wa Bulgaria kujadili tukio hilo, inasema televisheni ya BTV.
Chanzo - BBC Swahili