Mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Lukobe Edmond Petro kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro, Igidius Edmond (13) amejiua kwa kujinyonga kwa kamba ya manila huku sababu za kujinyonga zikiwa hazijafahamika.
Akizungumzia tukio hilo baba wa mtoto huyo, Edmond amesema kuwa mwanaye alijinyonga jana Jumapili Novemba 14, 2021 kwenye chumba cha dada zake wakati yeye akiwa amepumzika kwenye mti nje ya nyumba.
Baba huyo alisema kuwa mapema asubuhi mwanaye huyo aliamka akiwa na afya njema na furaha na baadaye alichukua daftari na kuanza kufanya kazi aliyopewa shule huku wakati dada zake wakijiandaa kwenda kanisani Jumapili.
“Hata yeye alijiandaa kwenda kanisani lakini ghafla aliwaambia dada zake kuwa hataweza kwenda kwa kuwa anafanya kazi aliyopewa shuleni, hivyo dada zake walijiandaa na kwenda kanisani na kumuacha chumbani akiwa na madaftari yake,” alielezea Edmond.
Alisema kuwa yeye aliendelea kupumzika kwenye mti mpaka mabinti zake wawili waliporudi kutoka kanisani ambapo walimuamsha na kumjulisha kuwa ndugu yao amejinyonga.
“Kiukweli sikuamini maana sikuweza kusikia purukushani yoyote nilikwenda ndani na kumkuta mwanangu akiwa ananing’inia kwenye kitanzi kamba ya manila na ndipo nilipoita majirani ambao walipiga simu Polisi,” alisema baba wa mtoto huyo.
Social Plugin