Na Ali Lityawi - Kahama
MKAZI wa Kata ya Nyihogo katika Manispaa ya Kahama, Maduhu Tarasisi Chubwa (60),amehukumiwa kwenda Jela maisha baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka miwili.
Hukumu hiyo ilitolewa Novemba 5,2021 na Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Kahama,Christine Chovenye, baada ya kukubaliana na ushahidi wa upande wa mashtaka na kumtia hatiani mshtakiwa.
Hakimu Chovenye alisema ametoa adhabu hiyo baada ya kukubaliana na ushahidi wa upande wa mashitaka ambao haujaacha shaka,kuwa mshtakiwa alitenda kosa kinyume cha kifungu namba 130(1)na (2) (e) na kifungu cha namba 131(3) kinyume na kanuni ya adhabu namba 16 kama kilivyorekebishwa RE 2019.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha mashtaka wa serikali, Mercy Ngowi,kuwa mtuhumiwa huyo alimbaka Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mwili,mnamo tarehe 11/10/2021,majira ya mchana katika eneo la Nyihogo.
Hata hivyo wakati wa mwenendo wa kesi hiyo mshatakiwa Chubwa aliposomewa shitaka hilo mbele ya mahakama hiyo alikana kutenda kosa hilo.
Akitoa hukumu hiyo,Hakimu Covenye,alisema mahakama imejiridhisha na ushahidi wa walioshuhudia kitendo hicho kutoka katika eneo la Chumba jirani na alichokuwa akiishi Mtuhumiwa,ikiwa ni pamoja na mtoto huyo kukutwa na mbegu za kiume sehemu za siri.
Chovenye aliieleza kuwa upande wa mashitaka ulifunga ushahidi uliotolewa na Dkt, Idd Ramadhani kutoka katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, aliyemfanyia uchunguzi wa kitabibu binti huyo na kumkuta akiwa na mbegu za kiume na michubuko katika sehemu zake za siri.
Aidha Hakimu huyo alieleza ushahidi mwingine ulikuwa ni wa mazingira pamoja na majirani ambao waliutoa mahakamani na hivyo Mahakama hiyo kujiridhisha na ushahdi huo na kutoa adhabu hiyo ya mshtakiwa kutumikia kifungo cha maisha jela.
Kabla ya kutolewa hukumu hiyo,Mwendesha mashitaka Ngowi,aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa huyo kwani kitendo alichomfanyia mtoto huyo hakivumiliki katika jamii,na kwamba kimesababisha majeraha makali na makovu ya milele kwa mtoto huyo mdogo.
Hata hivyo mtuhumiwa huyo Maduhu Tarasisi Chubwa alipotakiwa kujitetea mahakamani hapo alisema kuwa yeye ni mzee na kuiomba Mahakama kumpunguzia adhabu na mahakama hiyo kuamua kutoa adhabu kali iwe fundisho kwa watu wenye tabia kama hizo.
Social Plugin