Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Ruvuma, Pili Mande
Na Andrew Chatwanga,Ruvuma
Jeshi la polisi mkoani Ruvuma linawasaka wanaume wawili kwa tuhuma za kuwaua wake zao ambapo mmoja amemkata na shoka na mwingine kumpiga mpaka kumuua.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Pili Mande amelitaja tukio la kwanza limetokea Oktoba 31 mwaka huu mchana katika Mtaa wa Mateka manispaa ya Songea.
Mande amesema inadaiwa kuwa marehemu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa kabla ya kifo chake alikuwa kwenye sherehe nyumba ya jirani yao akiwa amesimama na mwanaume mwingine kwenye sherehe hiyo na ndipo alipokutwa mme wake ambaye jina naye limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi.
Alisema baada ya kukutwa na mume wake huyo akiwa amesimama na mwanaume mwingine alianza kumshambulia kwa kumshushia kipigo katika maeneo mbalimbali ya mwili na kumsababishia Bandama kupasuka jambo ambalo lilipelekea kuvuja kwa damu nyingi hadi kifo kutokea.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Mande alifafanua kuwa inadaiwa mtuhumiwa baada ya kumshushia kipigo mke wake na kugundua kuwa ameua alimchukua mtoto wake na kwenda kumtelekeza kwa babaake mzazi ambaye jina lake limehifadhiwa kisha baadaye alikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Aidha Kamanda Mande amelitaja tukio la pili kuwa limetokea Oktoba 28 mwaka huu usiku huko katika kijiji cha Mageuzi Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambapo mwanamke mmoja ambaye jina lake halikutajwa mwenye umri wa miaka 33 inadaiwa kuwa alipigwa na shoka kichwani kutokana na mume wake kumtuhumu mke wake kuwa ana mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine.
Alieleza kuwa wapenzi hao walikuwa wametengana lakini siku ya tukio bwana alimlaghai mpenzi wake kwa kummywesha pombe kisha kwenda nae nyumbani kwake ambako baadae alimshushia kwa kumipiga na shoka kichwani na kumsababishia kifo.
Mtuhumiwa baada ya tukio hilo inadaiwa kuwa aliuza mahindi na maharage ambayo alipata nauli kisha alikimbia na kutokomea kusikojulikana na polisi inaendelea kumsaka.
Jeshi la polisi limesema kutokanana mtukio hayo kukithiri mkoani humo limekemea na kulaani vikali kwa mtu yeyote atakayebainika kumshambulia kwa kumpiga mke wake au mume wake atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali wadhifa wake kwa kuwa mashambulio hayo yanaleta madhara makubwa kwa familia na jamii kwa ujumla na si vingninevyo.
Katika hatua nyingine Mande amewataka wale wanaomiliki silaha kinyume sheria wajisalimishe wenyewe kwenye vituo vya polisi vivyokuwa jirani kuanzia Novemba mosi hadi Novemba 30 mwaka huu.
Social Plugin