WAZAZI NA WALEZI WAASWA KULEA WATOTO KATIKA MAADILI MEMA


Mkurugenzi wa Shirika la Hope For Girls and Women Tanzania Rhobi Samwelly

Na Frankius Cleophace - Mara.

Wazazi na walezi hapa nchini wameaswa kulea watoto wao katika maadili mema ikiwa ni pamoja na kuwajengea mazingira rafiki katika ukuaji wao.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Shirika la Hope For Girls and Women Tanzania lililopo wilayani Butiama Mkoani Mara Rhobi Samwelly wakati akizungumzia siku ya mtoto kimataifa ambayo ufanyika kila Novemba 20 kila mwaka.

Rhobi aliseama kuwa wazazi wote wawili Baba na Mama wana jukumu la kulea watoto wao bila ubaguzi ili kuwajengea misingi bora katika makuzi yao kuanzia ngazi ya familia hadi kwenye jamii inayowazunguka.

“Ukiangalia suala la malezi mara nyingi mama ndiye anayebeba majukumu yote hivyo sasa ifike hatua jamii ibadilike wanaume waweze kushiriki vyema suala la malezi bila kumwachia mtu mmoja” alisema Rhoby.

Rhobi aliongeza kuwa kumekuwepo na vitendo vya ukatili na wakati mwingine vinawakumba watoto wadogo kuanzia miaka sifuri hadi miaka mitano nakuendelea jambo ambalo amelaani vikali kupitia siku ya mtoto kimataifa nakuomba jamii kuendelea kulinda haki za watoto bila kuwabagua.

“Ukatili upo wa aina mbalimbali sisi kama kituo cha matumaini hapa Butiama tumekuwa tukipokea watoto ambao wamefanyiwa ukali sasa jamii ifike hatua ithamini watoto wote ni sawa bila kubagua huyu ni mtoto wa kiume au wa kike kama ni kazi waote wapewe kazi sawa kama ni kupelekwa shule wote wapelekwe shule jamii iondokane na mila kandamizi kwa waoto hususani wa kike” alisema Rhobi.

Kwa upande wake Marwa Mwita mkazi wa wilaya ya Tarime alisema kuwa jukumu kubwa la kulea watoto mara nyingi ananachiwa mama hivyo sasa jamii ifike hatua ibadili mitazamo ili watoto waweze kupata malezi kutoka pande mbili.


“Imefikia hatua mpaka wanaume wengine hawatoi matumizi kwenye familia zao kwa sababu wanawake wanajishughulisha na kazi ndogondogo huku wakilea watoto bila kusaidiwa na wanaume wao mfano maaeneo ya vijijini wanaume wengi wanakunywa pombe za kienyeji wanashindwa kutunza familia zao” alisema Marwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post