****
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limesema linafanya uchunguzi kuhusu tukio la mauaji ya kijana ambaye hajafahamika jina wala makazi yake (25-30) ambaye amekutwa ameuawa na kutobolewa macho usiku wa kuamkia leo Jumamosi Novemba 6,2021 katika ghuba la kuhifadhia uchafu la Ngokolo Mitumbani Mjini Shinyanga.
Akizungumza na Malunde 1 blog, Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga ACP George Kyando amesema bado wanafanya upelelezi ili kuwabaini chanzo cha mauaji na wahusika wa mauaji hayo
"Jeshi la Polisi tumefika eneo la tukio, tumekuta pembeni ya mwili wa marehemu kuna vyuma ambavyo huenda ndivyo vimetumika kufanyia mauaji. Tunaendelea kufanya upelelezi ili kujua chanzo cha tukio lakini pia kuwabaini wahusika wa mauaji haya",amesema.
"Tumechukua mwili wa marehemu na tuumepeleka hospitali kwa ajili ya uchunguzi, bahati mbaya huyu mtu hajulikani jina wala makazi yake, hatujajua kama aliuawa pale, au aliuawa mahali pengine akaja kutupwa pale, tunaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini nini hasa hasa kilitokea",ameongeza Kamanda Kyando.
Baadhi ya mashuhuda waliofika eneo la tukio wamesema wameukuta mwili wa kijana huyo akiwa ameuawa kinyama na kutobolewa macho na watu wasiojulikana majira ya saa moja asubuhi kisha Jeshi la polisi lilifika na kuuchukua mwili huo na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.
Social Plugin