Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha
Mwanafunzi wa kidato cha Tatu katika shule ya Sekondari Suye na Mkazi wa Kijenge katika halmashauri ya jiji la Arusha Evance Florian (17) amefariki dunia baada ya kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake na Mwanafunzi wa Chuo cha ufundi Arusha (ARUSHA TECHNICAL COLLEGE) Ibrahim Shaban (18) kutokana na ugomvi uliosababishwa na kudaiana fedha kiasi cha Tsh. 3000/=.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo tukio hilo limetokea Novemba 13, 2021 muda wa saa 05:30 asubuhi katika maeneo ya hospitali ya rufaa ya Mount Meru Jijini Arusha ambapo Evance Florian (17) Mwanafunzi wa kidato cha Tatu katika shule ya Sekondari Suye na Mkazi wa Kijenge katika halmashauri ya jiji la Arusha alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospital ya rufaa ya Mount Meru baada ya kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
"Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliosababishwa na kudaiana fedha kiasi cha Tsh. 3000/= na kijana mmoja aliyefahamika kwa majina Ibrahimu Shabani (18) Mwanafunzi wa Chuo cha ufundi Arusha (ARUSHA TECHNICAL COLLEGE)",amesema Kamanda Masejo.
"Mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na pindi upelelezi utakapo kamilika jalada litapelekwa ofisi ya Taifa kwa hatua zaidi za kisheria. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hopitali ya rufaa ya Mount Meru",ameongeza.
Katika tukio jingine, Kamanda Masejo amesema Novemba 12, 2021 muda wa 11:35 jioni kitongoji cha ANTSA kijiji cha Mang’ola kata ya Mang’ola tarafa ya EYASI wilaya ya Karatu katika Mkoa wa Arusha askari wakiwa doria walifanikiwa kumkamata mtu mmoja jina (limehifadhiwa) akiwa na lita mia tatu na tano (305) za pombe haramu ya gongo (pombe ya moshi) ikiwa katika nyumba yake.
"Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwakamata wale wote wanajihusisha na biashara hii haramu. Aidha mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa katika vyombo husika kwa hatua zaidi za kisheria.
Nitoe wito kwa wanachi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao ili kutokomeza kabisa uhalifu katika Mkoa wetu",amesema Kamanda Masejo
Social Plugin