GGML YAENDELEZA UDHAMINI WA UPASUAJI MIDOMO SUNGURA


Meneja wa Afya, usalama na mazingira kutoka GGML, Dk. Kiva Mvungi akiwa amembeba mtoto anayetarajiwa kufanyiwa upasuaji wa midomo sungura.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo akiwa kambeba mtoto anayejiandaa kupata huduma ya upasuaji wa mdomo sungura inayofadhiliwa na GGML kwa kushirikiana na Rafiki Surgical Mission.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo (kulia) akisalimiana na wazazi na walezi wa wagonjwa wa mdomo sungura (kushoto) ambao wanatarajiwa kupata matibabu katika Hospitali ya Sekou Toure jijini Mwanza.
**

Na Mwandishi wetu

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa kushirikiana na Rafiki Surgical Mission ya Australia kwa mara nyingine mwaka huu imeendeleza udhamini wake wa kusaidia kugharamia upasuaji na matibabu ya wagonjwa 25 wa midomo Sungura katika Hospitali ya Sekou Toure jijini Mwanza mwezi huu.

Msaada huu umekuwa ukitolewa kwa zaidi ya muongo mmoja sasa tangu mwaka 2002 ukitoa matibabu kwa wagonjwa zaidi ya 1,717 wakiwemo watoto na watu wazima kutoka maeneo yanayozunguka mgodi.

Tatizo la midomo Sungura ni changamoto ya kidunia na bahati mbaya ni tatizo linalowakumba zaidi watoto kuzunguka eneo la Ziwa Victoria ambapo kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) inapatikana.

Chanzo cha midomo sungura hakijulikani lakini inasemekana ni matokeo ya jeni na sababu za kimazingira.

Akizungumzia udhamini huo jana mjini Geita kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Meneja Mwandamizi anayeshughulikia Afya, usalama, mazingira na mafunzo, Dk. Kiva Mvungi amesema GGML inatoa udhamini huu ili kurejesha matumaini na tabasamu kwa watoto na watu wazima.

Amesema udhamini huo utagharimia matibabu, malazi na usafiri katika kipindi chote ambacho watapatiwa matibabu hayo kwenye Hospitali ya Sekou Toure jijini Mwanza.

“Udhamini huu unaendana na tunu na ahadi za kampuni hiyo ambapo afya ni kipaumbele cha kwanza cha kusaidia jamii inayozunguka mgodi,’ amesema.

Dk. Mvungi ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 17 ambayo GGML imegharimia matibabu hayo, wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji wamepata matumaini mapya na maisha yao yamekuwa tofauti kabisa.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Wilson Shimo amesema kutoa ufadhili huo wa matibabu ya upasuaji wa midomo sungura kwa wagonjwa hao uliofanywa na GGML kwa kushirikiana na Rafiki Surgical Mission, ni mwendelezo wa GGML kusaidia sekta ya afya katika wilaya hiyo na wananchi.

Shimo amewapongeza wananchi waliojitokeza hadharani kuleta watoto wao kufanyiwa upasuaji na kuachana na imani potofu za kuwaficha ndani ya nyumba na kuendelea kupata matatizo bila kutibiwa.

Amewataka wananchi kuachana na tabia ya kuficha walemavu ndani hasa watoto badala yake wajitokeze kwa ajili kutibiwa kama watu hao 25 waliojitokeza na kupata ufadhili wa matibabu kutoka mgodi wa GGML kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho ya midomo yao.

GGML imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo mkoani Geita. Kwa kushirikiana na Serikali imefanikiwa kuwekeza kiasi cha fedha za kitanzania bilioni 50 kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo ya afya, elimu na miundombinu.

Kampuni ya GGML pia imelipa zaidi ya trilioni 3.9 za kitanzania kama kodi serikalini tangu kuanza shughuli zake Mwaka 2000.
Mbali na kodi na fedha za wajibu wa kampuni kwa jamii,kampuni pia inao mpango wa kusaidia fursa za kukuza uchumi kwa wafanyabiashara wazawa ambapo kampuni hiyo imetumia jumla ya shilingi za kitanzania bilioni 67.6 katika manunuzi ya bidhaa na huduma kutoka kwa kampuni za kitanzania mwishoni mwa mwezi Septemba 2021.

Katika kuendeleza biashara za kitanzania kwenye mnyororo wa thamani ndani ya mgodi, kampuni ya GGML imeshirikiana na Baraza la Taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC) na kuwajengea uwezo wafanyabiashara zaidi ya 350 kutoka Geita kwa kuwapatia mafunzo na ujuzi mbalimbali.

Mapema mwaka huu, kampuni ya GGML iliibuka mshindi wa jumla katika kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini nchini Tanzania kwa Mwaka wa fedha 2019/2020 baada ya kunyakua tuzo katika vipengele vya uwajibikaji wa kampuni kwa jamii, mazingira,usalama, mlipaji bora wa mapato (kodi) na uendelezaji wazawa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post