MWIMBAJI maarufu wa Brazil ambaye pia mshindi wa tuzo la Grammy 2019 kwa Amerika ya Kusini, Marilia Mendonca (26) amefariki dunia baada ya ndege aliyokuwemo kupata ajali.
Watu wengine wawili ambao ni mjomba wake, producer wake na wengine kutoka kwenye crew yake nao wamepoteza maisha kutokana na ajali hiyo iliyotokea Kusini Mashariki mwa mji wa Minas Gerais, uchunguzi bado unaendelea kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Huyu ni miongoni mwa wasanii wakubwa sana nchini Brazil ambaye alikuwa akiimba muziki wa country maarufu kama sertanejo kwa Brazil, Mendonça alianza kujihusisha na muziki tangu akiwa mtoto na umaarufu wake ukaibuka mwaka 2016 na ngoma yake iliyokuwa ikizungumzia michepuko kwenye mahusiano, alifahamika kama “Queen of Suffering” ama Malkia wa Mateso.
Mwaka jana aliahirisha matamasha yake yote kutokana na kusambaa kwa janga la Corona, lakini ndiye alikuwa msanii aliyesikilizwa zaidi kwenye Mtandao wa Music wa Spotify na kutazamwa zaidi YouTube.
Mendonça, ambaye ameacha watoto wawili, alikuwa amepanga kufanya bonge la shoo jana Ijumaa jioni katika jiji la Caratinga, ambalo lipo kilomita 12 pekee kutoka eneo alipopata ajali, muda mfupi kabla ya ajali aliposti video akijiandaa na safari.
Licha ya taarifa za awali za mmoja wa wafanyakazi wake aliyedai kuwa Mendoca ametoka akiwa mzima, simanzi iliibuka baada ya staa wa Soka wa Brazilian, Neymar kuandika kwenye mtandao wake wa Twitter kuwa: “Siwezi kuamini, siwezi”. Mwanamuziki aitwaye Anitta naye aliandika: “Siwezi kuamini huu msiba. Nataka kuamini kwamba bado kuna matumaini”.