Elias Ramadhani Masumbuko
Gulamhafeez Abubakar Mukadam
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi Manispaa ya Shinyanga wamempendekeza Elias Ramadhani Masumbuko kuwania kiti cha Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga kuziba nafasi ya David Mathew Nkulila aliyefariki dunia Agosti 23,2021.
Katika uchaguzi wa kura za maoni uliofanyika leo Alhamis Novemba 11,2021 Elias Ramadhani Masumbuko ambaye ni Diwani wa kata ya Chamaguha amepata kura 14 dhidi ya Gulamhafeez Abubakar Mukadam wa kata ya Mjini aliyepata kura 10.
Uchaguzi huu wa Kura za maoni umefanyika baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa iliyokutana katika kikao maalum Jumapili Novemba 7, 2021 Ikulu ya Chamwino, Jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwateua Ndugu Gulamhafeez Abubakar Mukadam na Elias Ramadhani Masumbuko kugombea kiti cha Umeya katika Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza na Malunde 1 blog, Katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Agnes Bashemu amesema uchaguzi huo wa kura za maoni umefanyika leo ambapo wajumbe waliopiga kura ni 24 kati ya 25 ambapo Gulam Hafeez Mukadam amepata kura 10 huku Elias Masumbuko akiibuka mshindi kwa kupata kura 14.
“Mara baada ya uchaguzi huu wa kura za maoni kumpata Meya wa Manispaa ya Shinyanga kupitia Chama Cha Mapinduzi, Jina la Elias Ramadhani Masumbuko litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga kisha madiwani watampigia kura za Ndiyo au Hapana",amesema Bashemu.
Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Shinyanga lina Madiwani 17 kutoka kata 17 na Madiwani sita wa Viti Maalum ambao wote ni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Elias Ramadhani Masumbuko amekuwa Mwenyekiti wa mtaa wa Sanjo kata ya Chamaguha kwa kipindi cha miaka 11 (awamu ya kwanza 2000-2005, awamu ya pili 2010-2015 na awamu ya tatu 2020) kabla ya kuchaguliwa kuwa Diwani wa kata ya Chamaguha katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 huku Gulamhafeez Abubakar Mukadam ambaye amekuwa Diwani wa kata ya Mjini kwa zaidi ya miaka 10 amewahi kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga kwa miaka 10 (2010-2015, 2015- 2020).
Mwaka 2020 David Mathew Nkulila alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga baada ya vikao vya juu vya CCM kurudisha jina lake na kuondoa jina la Gulamhafeez Abubakar Mukadam.
David Mathew Nkulila alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Novemba 24 Mwaka 2020 na alitumikia nafasi ya Meya kwa kipindi cha miezi 10 hadi umauti ulipomkuta usiku wa kuamkia Jumatatu Agosti 23,2021 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni maradhi ya moyo yaliyokuwa yanamsumbua.