WAZIRI MKUU MGENI RASMI MAADHIMISHO MIAKA 10 YA LSF


Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala (katikati) akiwa na mnufaika wa mradi wa upatikanaji wa haki, Asia Shemdoa pamoja na wadau wengine wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya LSF yanayotarajiwa kufanyika Novemba 11, 2021.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya LSF yanayotarajiwa kufanyika Novemba 11, 2021.


Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika madhimisho ya miaka 10 ya Shirika la Legal Services Facility (LSF) yanayotarajiwa kufanyika tarehe 11 Novemba mwaka huu jijini Dar es Salaam.

LSF ni shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya kukuza upatikanaji wa haki nchini Tanzania kupitia utekelezaji wa program ya upatikanaji wa haki.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana tarehe 4 Novemba, 2021, Afisa Mtendaji Mkuu wa LSF, Lulu Ng’wanakilala amesema tukio hilo linalenga kusherehekea matokeo na mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa program mbalimbali.

Ametaja progamu hizo kuwa ni upatikanaji wa haki nchini Tanzania (Access to Justice Program), Mradi wa Uwezeshaji wa Kisheria Maeneo ya Mijini (Urban Legal Empowement Project) pamoja na miradi mingine ya kimkakati.

“LSF imejikita katika maeneo makuu manne ikiwemo; upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kupitia kwa watoa huduma za msaada wa kisheria takriban 4,000; kuwa na jamii iliyowezeshwa kisheria; kuboresha mazingira Rafiki ya upatikanaji wa huduma bora za msaada wa kisheria; pamoja na kujenga mazingira ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria endelevu katika ngazi ya kitaasisi,” amesema.

Aidha, amesema tukio hilo linakwenda sawia na maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria, ambapo wadau nchi nzima hususani wasaidizi wa kisheria wanaendelea kutoa bure katika kila wilaya nchi nzima.

Amesema katika kipindi cha miaka 10, LSF imetoa ruzuku kwa mashirika yanayotoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria zaidi ya 200 Tanzania bara na Visiwani Zanzibar. 

Amesema LSF imekuwa ikishirikiana na serikali katika ngazi ya chini mpaka juu serikalini kupitia Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI) na kufanikiwa kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi milioni sita na kjutatua migogoro 90,000 kwa mwaka.

“Pia imekuwa ikifanya kazi na Wizara ya Mambo ya Ndani katika mradi wa haki jinai (Criminal Justice Project) ambao unatekelezwa na shirika mdau wetu wa kimkakati ENVIROCARE wakati kwa upande wa Jeshi la Polisi Tanzania, LSF inashirikiana nao kupitia makubaliano yaliyolenga kuwezesha zoezi la kupitia upya mwongozo wa jeshi hilo (General Police Orders – PGO,” amesema.

Amesema LSF imekuwa ikifanya kazi na Wizara ya Afya katika mpango wa kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na Watoto.

Vilevile LSF imekuwa ikifanya kazi na Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Visiwani Zanzibar katika kukuza upatikanaji wa haki visiwani humo pamoja na kuboresha sera ya wasaidizi wa kisheria Zanzibar.

Amesema katika kutambua tija iliyo nayo sekta ya kilimo nchini Tanzania, katika kipindi cha miaka 10, LSF imekuwa na makubaliano na Benki ya Taifa ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa kusaidia kuvijengea uwezo wakulima, vyama vya msingi vya wakulima (AMCOS) na wajasiriamali wengine katika sekta ya kilimo.

“Kubwa zaidi katika kipindi hiki, LSF ni sehemu ya mafanikio ya upatikanaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria iliyopitishwa mwaka 2017 ili kuwatambua rasmi wasaidizi wa kisheria nchini.

“Hivyo, tukielekea kuadhimisha miaka 10 ya LSF, tunawashukuru wadau wetu muhimu wa maendeleo ikiwemo DANIDA, Umoja wa Ulaya, UKAID, DFiD, ambao tumekuwa nao katika hatua mbalimbali za safari hii katika kukuza upatikanaji kwa watu wote hususani wanawake na Watoto,” amesema Afisa Mtendaji huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post