Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHUO CHA NGOZI DIT MWANZA KINAKABILIWA NA IDADI NDOGO YA WANAFUNZI

Na Dinna Maningo, Mwanza
CHUO kinachotoa mafunzo ya kuchakata ngozi (Leather Processing) na kutengeneza bidhaa za ngozi (Leather Products Technology) ambacho kipo chini ya Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT) tawi la Mwanza kinakabiliwa na idadi ndogo ya wanafunzi.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi, Fundi Bidhaa za ngozi,Ramadhani Khalfani kutoka Taasisi hiyo anasema kuwa DIT Mwanza ndiyo chuo pekee Tanzania mzima kinachotoa mafunzo ya ngozi kwa ngazi ya Stashahada (Diploma).

Anasema kuwa licha ya kuwa ni chuo pekee kinachotoa mafunzo kwa ngazi hiyo,wanafunzi walioko mwaka wa kwanza ni 12 kati ya hao wavulana ni 10 na wasichana wawili.

Khalfani anasema kuwa walioko mwaka wa pili ni 31 kati ya hao wavulana ni 19 na wasichana ni 12 na wa mwaka watatu walikuwa watano kati yao mvulana mmoja alifeli mtihani na kubaki wanne wavulana watatu na msichana mmoja.

" Kwa upande wa uchakataji wa ngozi kozi imeanzishwa mwaka huu ngazi ya Diploma ila hadi sasa ameripoti mwanafunzi mmoja,sifa za kujiunga ni aliyemaliza kidato cha nne au sita na awe amefaulu masomo ya sayansi ikiwemo Kemia,Fizikia,Hesabu na Kingereza",anasema Khalfani. 

Anaeleza kuwa kumekuwa na mwamko mdogo kwa wananchi wakiwemo wa kike kutojitokeza kujiunga na mafunzo ya uchakataji na utengenezaji wa bidhaa za ngozi licha yakwamba mafunzo hayo yanatoa ujuzi wakumwezesha mtu kuajiriwa au kujiajiri.

Anasema sababu zinazochangia kuwepo kwa idadi ndogo ya wanafunzi ni kozi hizo kutolewa kwa ufaulu wa masomo hayo ya sayansi,uelewa mdogo kuhusu ngozi na bidhaa zake na chuo hicho kutofahamika.

Elizabeth Julius mwanafunzi anayesomea utengenezaji wa bidhaa za ngozi katika chuo hicho anasema kuwa  sababu ya wasichana kutojiunga na mafunzo ni kuogopa masomo ya sayansi lakini pia kuiona kozi hiyo kuwa inawahusu wanaume.

"Mimi natokea mkoa wa Geita nilihitimu kidato cha nne,serikali ikanipanga kuja DIT kusomea ujuzi wa kutengeneza bidhaa za ngozi,huko sekondari wanafunzi wanakwepa sayansi hasa wa kike mimi naipenda kazi hii tunaiomba serikali itupatie vitendea kazi vya kujifunzia chereheni ni chache na mashine  hali inayosababisha tusifanye mazoezi kwa vitendo inavyohitajika.

Anawashauri wanafunzi walioko Sekondari kutoyaogopa masomo ya Sayansi kwa kile alichoeleza kuwa masomo ya sayansi yana fursa nyingi katika ajira nakwamba fani ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi si kazi ya mwanaume tu hata wanawake wanaweza.

Muhitimu wa Stashahada ya Teknolojia ya bidhaa ya ngozi Jackson Peter aliyehitimu mwaka jana anasema kuwa bado kuna changamoto ya wataalamu wa kutengeneza bidhaa za ngozi nakwamba wamehitimu wanafunzi watano pekee.

"DIT Mwanza ndiyo inatoa elimu ya Teknolojia ya ngozi kwa ngazi ya diploma,nilihitimu elimu ya kidato cha sita nikajiunga na diploma ya teknolojia ya ngozi ,natamani ningeendelea na shahada (degree) lakini haipo hiyo kozi,naishukuru serikali kwa kuanzisha hiki chuo,elimu niliyoipata nitaieneza kwa wengine" anasema Peter.

Mkazi wa Pasiansi wilaya ya Ilemela -Mwanza Annastazia Yusuphu anasema kuwa licha ya chuo hicho kuwa kwenye wilaya hiyo hakifahamiki hivyo anaiomba serikali kukitangaza kupitia wataalamu wake kwenye vyombo vya habari,kwenye makanisa, misikiti, vikao vya madiwani na kupitia mikutano ya wananchi ili kutoa fursa kwa vijana kujiunga na masomo.

"Hicho chuo ndiyo nasikia kutoka kwako mimi nimeishi Mwanza miaka 15 sijawahi kufahamu kama kuna chuo cha Ngozi, ni vyema serikali kupitia wataalamu wake wakazunguka mikoani na kwenye wilaya na shule zote za sekondari kukitangaza chuo,sidhani kama Watanzania wengi wanakifahamu hicho chuo,serikali ijitahidi kuvitangaza vyuo vyake vikijulikana vitapata wanafunzi wengi" anasema Yusuphu.

Khalfani anasema kuwa awali chuo hicho kilikuwa chini ya Wizara ya Viwanda kilichojengwa 1984,kilijulikana kama TILT (TANZANIA INSTITUTE OF LEATHER TECHNOLOGY) na kwa miaka hiyo hakikufanya uzalishaji kama ilivyotakiwa hivyo mwaka 1990 kiwanda kilifungwa na baadae kubinafsishwa.

Mtaalamu huyo wa ngozi anasema kuwa Mei, 1,2010,serikali ya awamu ya nne iliyokuwa inaongozwa na aliyekuwa Rais Dkt Jakaya Kikwete, kiwanda kilirudishwa Serikalini na DIT walikabidhiwa rasmi kuendesha mafunzo.

Anasema kuwa mwaka 2010-2012 chuo kilifanyiwa ukarabati ambapo Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Benk ya CRDB walikuwa ndiyo wadau wakubwa waliodhamini ukarabati wa majengo.

"Mwaka 2011 hadi 2014 COSTECH ilisaidia kufanya ukarabati wa majengo ya  DIT Mwanza kwa kubadilisha paa za majengo ya hosteli,karakana,careteria,madarasa pamoja na majengo ya maabara ambapo ilitoa milioni 80 kukarabati majengo" anasema Khalfani.

Anasema kuwa 2016 chuo kilianza fani ya Stashahada ya utengenezaji wa bidhaa za Ngozi na Teknolojia ya Sayansi ya Maabara,na sasa inatoa na kozi ya uchakataji wa ngozi nakwamba malengo ya chuo ni kuwa kitovu cha umahiri katika teknolojia ya ngozi.
Bidhaa zitokanazo na ngozi kutoka chuo cha DIT Mwanza
Bidhaa zitokanazo na ngozi kutoka chuo cha DIT Mwanza
Wanafunzi wa DIT Mwanza wakielekezwa namna ya kutumia mshine ya kukata ngozi inayoitwa click/ pressing machine

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com