Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu akitoa sakramenti ya ubatizo leo katika kanisa kuu la mama mwenye Huruma Parokia ya Ngokolo Jimbo la Shinyanga.
Na Samir Salum - Shinyanga
Askofu wa kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu ameendelea kuwasisitiza vijana kutokubali kutumiwa kuvuruga amani ya nchi na badala yake watumie nguvu walizonazo kuujenga Ufalme wa Mungu.
Askofu Sangu ametoa rai hiyo leo wakati akiongoza Misa takatifu ya kufunga mwaka wa kanisa iliyofanyika katika kanisa kuu la Mama Mwenye Huruma Ngokolo mjini Shinyanga ambayo imekwenda pamoja na kufunga kongamano la kijimbo la Vijana Wakatoliki wafanyakazi VIWAWA.
Amesema mara nyingi vijana wamekuwa wakitumiwa kufanikisha mipango ambayo imekuwa ikihatarisha hali ya amani katika mataifa mbalimbali jambo ambalo wanapaswa kulikataa na badala yake watumie nguvu na karama walizonazo katika kuujenga ufalme wa Mungu.
“Mara nyingi vijana wanatumiwa vibaya na watu ambao hawana nia njema kwa sababu wana nguvu sasa wanaweza kutumia nguvu zao vibaya,niwasihi vijana tumieni nguvu zenu katika kujenga ufalme wa mungu kwa kuwa chimbuko la haki,amani,upendo na umoja mahali kote duniani” ,amesema Askofu Sangu.
Askofu Sangu amewataka Watanzania kutochoka kumwomba Mungu ili aendelee kuimarisha misingi ya haki,amani,upendo na mshikamano hatua ambayo itasaidia kuliepusha taifa na hali ya migogoro na umwagaji damu ambao unatokea katika mataifa mengine kwa sababu tu ya ubinafsi wa watu wachache.
Kwa upande mwingine Askofu Sangu amewapongeza Wanawake Wakatoliki Tanzania WAWATA jimbo la Shinyanga kwa namna ambavyo wamejitoa katika kulilea shirika jipya la watawa la kijimbo la Mtakatifu Bikra Maria Mama mwenye Huruma ambalo limeanzishwa miaka michache iliyopita.
Amesema WAWATA wamefanya kazi kubwa katika kulilea na kulitunza shirika hilo hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto zilizopo.
“Nichukue Nafasi hii kuwashukuru sana WAWATA wamekuwa mstari wa mbele sana katika mwaka wote huu na miaka iliyopita katika kulitiunza na kulilea shirika letu la Bikira Maria Mama wa Huruma”, amesema Askofu Sangu.
Wakati huo huo askofu Sangu amewaongoza waamini kusali kuliombea taifa ili lipate mvua za kutosha kutokana na hali ya hewa kwa mwaka huu kutokuwa ya kuridhisha ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alioutoa kwa viongozi wa dini hivi karibuni jijini Mwanza.
Social Plugin